Home » images »

Acacia yasaini mikataba ya hati fungani ya mazingira

 

Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imetiliana saini na Kampuni ya Acacia Mining Plc, mikataba ya hati fungani kwa ajili ya ukarabati wa mazingira kwa migodi yake yote nchini.

Tukio hilo la utiaji saini lilifanyika jana Makao Makuu ya Wizara ambapo mikataba hiyo ilisainiwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Makamu wa Rais wa Acacia, Deo Mwanyika.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akibadilishana mikataba ya Hati Fungani na Makamu wa Rais wa Kampuni ya Acacia Mining, Deo Mwanyika.

Akizungumza kabla ya utiaji saini huo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema Kampuni ya Acacia Mining ni ya kwanza kukamilisha mikataba ya hati fungani ya Mazingira kwa migodi yake yote kama Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 inavyoelekeza.

Akizungumza mara baada ya tukio hilo, Kaimu Kamishna Msaidizi anayesimamia Sehemu ya Ukaguzi wa Migodi, Mhandisi Noel Baraka alisema tukio hilo lipo kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ambayo inaitaka Migodi yote ya Kati na Mikubwa kuwa na mpango wa kufunga mgodi uliopitishwa na Kamati ya Kitaifa ya kusimamia ufungaji wa Migodi na kuweka hati fungani ya gharama zitakazotumika kukarabati mazingira ya mgodi huo.

Ujumbe kutoka Kampuni ya Acacia Mining; wa kwanza kulia ni Makamu wa Rais wa Acacia, Deo Mwanyika akifuatiwa na Mshauri Mkuu wa Masuala ya Mazingira wa Kampuni ya Acacia, Diane Wamunza na Nector Foya.

Alisema, kwa mujibu wa Sheria hiyo, kila mgodi Mkubwa au wa Kati mara tu unapoanzishwa unatakiwa uanze mchakato wa maandalizi ya mpango wa ufungaji kwa lengo la kuhakikisha unarudisha mazingira kama yalivyokuwa kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji ama kuboresha zaidi ya ilivyokuwa.

Aliongeza kuwa lengo la kuwa na mikataba ya hati fungani ni Serikali kuwa na uhakika wa kurekebisha mazingira yaliyoharibika kwa sababu ya shughuli za uchimbaji madini hata kama Kampuni husika itashindwa kufanya hivyo kutokana na sababu yoyote.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza kabla ya tukio la utiaji saini wa mikata ya Hati Fungani ya Mazingira. Kulia ni Kaimu Kamishna wa Madini, Julius Sarota.

“Ili kuhakikisha eneo la mgodi linarudi kama lilivyokuwa au zaidi ya hapo, lazima kutakuwa na gharama inayohitajika; gharama hizo zinapaswa kuainishwa na mgodi na kupitishwa na Kamati ya Taifa ya Ufungaji wa Migodi baada ya kujiridhisha,” alisema.

Alisema gharama inafahamika mara baada ya Kamati hiyo inayohusika na taratibu za ufungaji wa migodi kujiridhisha kuwa kiasi kilichotengwa na mgodi husika kinatosha kwa shughuli hiyo.

Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Migodi nchini, Mhandisi Noel Baraka (wa pili kutoka kulia) akizungumza jambo wakati wa tukio la utiaji saini. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Kamishna wa Madini, Julius Sarota akifuatiwa na Afisa Mazingira, Innocent Makomba na Afisa Sheria, Phines Sijaona.

Alitaja baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo ni kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Ofisi ya Rais- Mazingira, Baraza la Usimamizi na Utunzaji wa Mazingira (NEMC), Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mkuu wa Mkoa na Wilaya husika, Mkurugenzi wa Halmashauri wa Wilaya husika pamoja na Wenyeviti wa Vijiji vinavyozunguka mgodi.

Naye Mshauri Mkuu wa Masuala ya Mazingira wa Kampuni ya Acacia, Rebbeca Stephen alisema kiasi cha fedha kilichowekewa hati fungani kwa shughuli hiyo kwa migodi yote ya Acacia ni Dola za Marekani 41,080,547 ambapo kwa mgodi wa Bulyanhulu ni Dola za Marekani 3,287,714, North Mara ni Dola za Marekani 19,164,344 na kwa mgodi wa Buzwagi ni Dola za Marekani 18,628,489 ambazo zimewekwa kwa mfumo wa ‘insurance guarantee’ kupitia Kampuni ya Metropolitan Tanzania Insurance Company Limited.

Imeandaliwa na:

Mohamed Saif,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz