Home » images »

ATOGS yakaribisha ushiriki kwenye mradi bomba la mafuta

 

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim, amesema  kuwa jumuiya inakaribisha makampuni mbalimbali nchini kujiunga na  jumuiya hiyo na kuwezeshwa kwenye ushiriki katika mradi wa  ujenzi wa bomba la mafuta  ghafi kutoka   Hoima nchini Uganda hadi  katika Bandari ya  Tanga nchini Tanzania.

Abdulrahim aliyasema hayo  leo kwenye mkutano wa waandishi wa habari  uliofanyika jijini Dar es Salaam na kushirikisha  Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, na watendaji kutoka Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) na  Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa pili kushoto) akifafanua jambo katika mkutano huo.

Alisema kuwa tayari baadhi ya makampuni yameshaanza kujiunga na jumuiya hiyo na kutaka watu binafsi wenye nia ya kushiriki katika utoaji huduma kwenye mradi wa bomba la mafuta kujiunga na jumuiya hiyo ili kuwezeshwa.

Alisema kuwa kazi kubwa itakayofanywa na ATOGS ni pamoja na kuwawezesha washiriki  kupata utaalam wa  utoaji wa huduma ikiwa ni pamoja  na namna ya kupata mikopo kwenye mabenki na  taasisi mbalimbali za kifedha.

Aidha, alipongeza jitihada za serikali katika kuwezesha uchumi wa viwanda kupitia mradi wa bomba la mafuta  hali inayoleta matumaini ya kuwa nchi  kutoka kwenye  orodha ya nchi masikini duniani na kuingia katika  orodha ya nchi  zenye kipato cha kati  ifikapo mwaka 2025 kama  Dira ya Maendeleo ya  Taifa, inavyofafanua.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye (katikati) akifafanua jambo katika mkutano huo. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim.

Alisisitiza kuwa  lengo la jumuiya ni kuwaunganisha watoa huduma wote  na kuwapa elimu ya namna bora ya utoaji  wa huduma  ili kuweza kushiriki kikamilifu katika mradi wa bomba la mafuta.

Aliongeza kuwa mradi  wa bomba la mafuta utaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kuanzia kwa mwananchi mmoja mmoja  hadi kwa  taifa kwa ujumla na kuwataka  wananchi hasa waishio katika mikoa itakayopitiwa na miundombinu  ya bomba la mafuta kuchangamkia  fursa na kuondokana na umasikini.

Aliendelea kutaja mikoa itakayopitiwa na miundombinu ya bomba la mafuta kuwa ni pamoja na Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Manyara na Tanga.

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watoa Huduma Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim (katikati) akielezea mikakati ya jumuiya hiyo ya kuwezesha wadau mbalimbali wataoshiriki katika utoaji wa huduma kwenye mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika Bandari ya Tanga nchini Tanzania kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 02 Agosti, 2017. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Godfrey Simbeye.

Wakati huo huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo alipongeza uanzishwaji wa  ATOGS na kusema kuwa jumuiya  hiyo imekuja wakati mwafaka wa mradi wa bomba la mafuta na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa zilizopo kupitia jumuiya hiyo.

Dkt. Pallangyo alitumia  fursa hiyo kuwakaribusha watanzania kujitokeza katika uzinduzi  wa mradi wa bomba la mafuta  ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika Bandari ya  Tanga nchini  Tanzania unaotarajiwa kufanywa na Marais Yoweri Museven wa Uganda na Dkt. John Magufuli  siku ya Jumamosi  wiki hii.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF). Godfrey Simbeye aliyataka makampuni yatakayopata tenda ya kutoa huduma kwenye mradi wa bomba la mafuta kufanya kazi kwa umahiri na uadilifu mkubwa kwa manufaa ya nchi.

“ Kutakuwepo na kazi nyingi sana zitakazotolewa kwa  watanzania hususan   huduma  kwa wakandarasi watakaojenga bomba,  umakini na uadilifu wa hali ya juu unahitajika ili kuleta sifa njema kwa nchi,” alisema  Simbeye

Aliishauri serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuweka mpango maaalum wa kutoa mafunzo wa namna ya kujenga mabomba ili  baadaye wataalam wa ndani ya nchi wafanye kazi ya kujenga mabomba na kupunguza  gharama.

Aliendelea kusema kuwa wakati serikali ikiimarisha mazingira mazuri ya uwekezaji nchini, mabenki yajiandae kutoa mikopo mara moja kwa makampuni yatakayopata tenda kwenye mradi wa bomba la mafuta.

Imeandaliwa na:

Greyson Mwase,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@mem.go.tz,                                                                               

Tovuti: mem.go.tz