Home » images »

Baraza la wafanyakazi: Waziri Muhongo aagiza kikao kikubwa cha wataalam

  • Watajadili maeneo mapya ya uwekezaji sekta ya madini
  • Ataka sekta za nishati, madini kuchangia ipasavyo uchumi wa viwanda

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amefungua Baraza la Wafanyakazi wa Wizara na kuiagiza Idara ya Madini kuandaa Mkutano mkubwa wa wataalam, Julai mosi mwaka huu, kujadili maeneo mapya ya uwekezaji katika sekta hiyo ili kuvutia wawekezaji hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa utekelezaji wa uchumi wa viwanda na katika Pato la Taifa.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, akizungumza katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara kilichofanyika hivi karibuni. Waziri Muhongo alikuwa Mgeni Rasmi katika kikao hicho na alishiriki kikao katika kundi lililokuwa Dodoma. Kikao hicho kiliendeshwa kwa kutumia teknolojia ya “Tele-Conference” na kilijumuisha makundi matatu katika vituo vya Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza.

Profesa Muhongo, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika mkutano husika uliofanyika Aprili 12 mwaka huu, katika vituo vitatu, Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam kwa kutumia teknolojia ya ‘Tele-Conference’, alimwelekeza Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje kuongoza kikao hicho cha wataalam ambacho pamoja na mambo mengine kitajadili na kuainisha aina mbalimbali za madini mapya na mahala yanakopatikana nchini.

Alielekeza kwamba, baada ya kikao hicho, kichapishwe kijitabu ambacho kitakuwa na maelezo ya aina zote za madini yanayopatikana nchini, hususan madini mapya yaliyo katika soko kwa sasa, ambayo ni pamoja na madini ya viwanda na ya ujenzi.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini (Dodoma), wakishiriki katika kikao cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni. Kikao hicho kiliendeshwa kwa kutumia teknolojia ya “Tele-Conference” na kilijumuisha makundi matatu katika vituo vya Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza.

Aidha, alibainisha kuwa, kijitabu hicho kioneshe mahala yanakopatikana madini husika ili kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta husika na hivyo kuchangia kikamilifu katika Pato la Taifa na kuwezesha ipasavyo uchumi wa viwanda.

“Tunataka kuwa nchi ya viwanda, hivyo sisi tuwasaidie wawekezaji wa ndani na nje kujua madini mapya yanayohitajika katika soko la Dunia kwa sasa pamoja na kuwaeleza ni mahali gani yanapatikana kwa wingi.”

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini (Dodoma), wakishiriki katika kikao cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni. Kikao hicho kiliendeshwa kwa kutumia teknolojia ya “Tele-Conference” na kilijumuisha makundi matatu katika vituo vya Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza.

Aliyataja baadhi ya madini mapya yanayohitajika zaidi katika soko la Dunia kwa sasa kuwa ni pamoja na Lithium na Graphite. Aidha alitia mkazo kuwa madini ya ujenzi yanahitajika sana kwa sasa. “Watu wengine wanadhani kokoto na mchanga siyo biashara; ni biashara kubwa sana.”

Alisema kuwa zama za watu kuchimba madini kwa kubahatisha, zimepitwa na wakati hivyo ni lazima Wizara ifanye jitihada za kuainisha ni wapi ilipo malighafi inayohitajika ili kusaidia ujenzi wa viwanda.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini (Dodoma), wakishiriki katika kikao cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni. Kikao hicho kiliendeshwa kwa kutumia teknolojia ya “Tele-Conference” na kilijumuisha makundi matatu katika vituo vya Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza.

Kuhusu kuainisha madini mapya, Profesa Muhongo alisisitiza kuwa siyo sahihi kama nchi kuendelea kushughulika na madini yaliyozoeleka peke yake kama almasi na dhahabu bali ni vema kwenda sambamba na mahitaji ya soko la Dunia kama ambavyo nchi nyingine ulimwenguni zinafanya.

“Kwa mfano, Lithium na Graphite zinahitajika sana kwa sasa kwa ajili ya Betri za Magari. Lazima tuwe wabunifu.”

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini (Dodoma), wakishiriki katika kikao cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni. Kikao hicho kiliendeshwa kwa kutumia teknolojia ya “Tele-Conference” na kilijumuisha makundi matatu katika vituo vya Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza.

Kwa upande wa nishati, Waziri Muhongo aliwataka wataalam wa sekta hiyo kuhakikisha wanaweka mkazo kwenye uzalishaji umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali tulivyonavyo kwa wingi nchini.

Alivitaja vyanzo hivyo kuwa ni gesi asilia, makaa ya mawe, maporomoko ya maji pamoja na nishati jadidifu inayojumuisha jua, upepo, jotoardhi, mawimbi ya Bahari na tungamotaka. “vyanzo hivi vipo kwa wingi nchini. Tuvitumie.”

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini (Dodoma), wakishiriki katika kikao cha Baraza hilo kilichofanyika hivi karibuni. Kikao hicho kiliendeshwa kwa kutumia teknolojia ya “Tele-Conference” na kilijumuisha makundi matatu katika vituo vya Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza.

Alisisitiza kuwa, kwa nchi ya viwanda, inayohitaji umeme mwingi, ni lazima mbinu mbalimbali za uzalishaji wa nishati hiyo zitumike ili kupata kiwango cha kutosha kinachotakiwa.

Waziri Muhongo pia, alitumia fursa hiyo kuwaasa watumishi wa Wizara kuzingatia suala la uaminifu kazini pamoja na kuwa wazalendo kwa nchi.

Meza Kuu, wakisikiliza hotuba ya wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, iliyokuwa ikiwasilishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara, Marcellina Mushumbusi (hayupo pichani). Kutoka kushoto ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa James Mdoe na Katibu wa Baraza la Wafanyakazi, Paschal Mduma.

Akizungumzia suala la Taasisi zilizo chini ya Wizara kuingia Mikataba ya Makubaliano (Memorandum of Understanding – MoU) na wawekezaji mbalimbali, Waziri Muhongo aliagiza kuwa ni lazima Taasisi zihakikishe zinaishirikisha Wizara (Waziri na Katibu Mkuu) pamoja na Mwanasheria Mkuu ili watoe maoni yao kabla ya kuingia katika MoU yoyote.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa James Mdoe, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo, alisisitiza kuwa maagizo yote yaliyotolewa na Waziri yatafanyiwa kazi ipasavyo.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini (Dodoma), wakifuatilia hotuba ya wafanyakazi iliyokuwa ikiwasilishwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Marcellina Mushumbusi (kwenye ‘screen’). Kikao hicho kiliendeshwa kwa kutumia teknolojia ya “Tele-Conference” na kilijumuisha makundi matatu katika vituo vya Dodoma, Dar es Salaam na Mwanza.

Akifafanua zaidi kuhusu utaratibu wa Taasisi za Wizara kusaini MoU za miradi mbalimbali, Profesa Mdoe alisema kwamba, maelekezo yaliyotolewa na Waziri Muhongo ni ya msingi sana na kwamba ana hakika utaratibu huo ukifuatwa, utaondoa kabisa matatizo mbalimbali ambayo yamekuwa yakijitokeza katika baadhi ya mikataba iliyoingiwa awali hususan inayohusu miradi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Awali, akisoma hotuba ya wafanyakazi wa Wizara, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara, Marcelina Mushumbusi, alimweleza Mgeni Rasmi kuwa, wafanyakazi wanatoa pongezi kwa Serikali kwa jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi.

Aidha, Mushumbusi aliuomba uongozi wa Wizara kuendelea kushirikiana na wafanyakazi katika hali zote ikiwa ni pamoja na kuendelea kuboresha maslahi yao.

Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, hufanyika mara moja kila mwaka kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu watumishi ikiwemo utendaji kazi.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@mem.go.tz,                                             

Tovuti: mem.go.tz