Home » images »

Darakuta kuingiza megawati 1.3 kwenye gridi ya Taifa

 

Imeelezwa kuwa kampuni ya uzalishaji  wa umeme kwa kutumia maji  (Darakuta Hydro Power Project) iliyopo Babati mkoani Manyara  inatarajia kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka Kilowati 370 hadi  Megawati 1.3 zitakazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa  na kupunguza  upungufu wa umeme nchini ifikapo mwaka 2021.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uzalishaji wa Umeme kwa kutumia Maji ya Darakuta, Raphael Bapsl (katikati) akionesha moja ya chanzo cha maji kinachotumika katika kuzalisha umeme.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji  wa kampuni hiyo, Raphael Bapsl wilayani Babati mkoani Manyara wakati  wa ziara ya wataalam  wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika wilaya hiyo, yenye lengo la kuangalia maendeleo ya miradi ya uzalishaji umeme na kubaini changamoto zake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Uzalishaji wa Umeme kwa kutumia Maji ya Darakuta, Raphael Bapsl (katikati) akionesha mfumo wa kuongozea mitambo ya kuzalisha umeme ya kituo hicho.

Akielezea historia ya mradi huo, Bapsl alisema kampuni yake ilianza kuzalisha umeme  wa Kilowati 50 mwaka 1995 na kuongeza kuwa Aprili mwaka 2016 kampuni ilianza kuliuzia  Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO) umeme unaoingizwa kwenye Gridi ya  Taifa.

Alisema mbali na umeme huo kutumika kwa matumizi ya nyumbani ambao ni kidogo hususan katika shughuli za kilimo na ufugaji ili kujiongezea kipato, kampuni yake huuza umeme wa ziada kwa TANESCO ili kuongeza kiasi cha  umeme katika wilaya ya Babati.

Alisisitiza kuwa ili Tanzania kuingia katika uchumi wa kati kupitia uwekezaji kwenye viwanda, nishati ya umeme wa uhakika inahitajika na kuendelea kusema kuwa kwa kutambua hilo kampuni yake imeweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ili kuhakikisha inachangia katika ongezeko la  umeme katika Gridi ya Taifa.

Imeandaliwa na:

Greyson Mwase,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz