Home » images »

Dkt. Pallangyo awaasa wazalishaji nguzo za umeme nchini kuzingatia ubora

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, anayeshughulikia masuala ya Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo, amekutana na wazalishaji wa nguzo za umeme nchini na kuwataka wazingatie viwango vya ubora katika uzalishaji wa nguzo hizo.

Kutoka kushoto ni Mjiolojia Mkuu kutoka Idara ya Nishati, Habass Ngulilapi, Mhandisi Nishati, Christopher Bitesigirwe na Mchumi, Paschal Mduma, wakiwa katika kikao cha Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo na wazalishaji wa nguzo za umeme nchini (hawapo pichani).

Dkt. Pallangyo alikutana na Ujumbe wa wazalishaji hao wanaounda Umoja wao ujulikanao kama African Forestry (AF) Julai 24, mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma.

Alisema kuwa kwa sasa Serikali imeazimia kutumia nguzo za umeme kutoka kwa wazalishaji wa ndani ya nchi pekee na kuachana na uagizaji wa nguzo nje ya nchi, hivyo ni vyema wazalishaji hao wakazingatia vigezo vyote vya ubora ili kutoiangusha Serikali.

Sehemu ya wazalishaji wa nguzo za umeme nchini, walioshiriki kikao baina yao na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (hayupo pichani), wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara, mjini Dodoma, Julai 24 mwaka huu.

Vilevile, Naibu Katibu Mkuu, aliwakumbusha wazalishaji hao kuhakikisha wanazalisha nguzo za kutosha kuweza kutosheleza mahitaji yake kwa nchi nzima.

“Serikali inaendelea na zoezi la usambazaji umeme vijijini kwa mikoa mbalimbali kote nchini lakini pia wananchi walioko mijini wanaendelea kuunganishiwa huduma hiyo muhimu. Kwa hivyo, nguzo za kutosha na zenye ubora wa hali ya juu zinahitajika,” alisisitiza.

Sehemu ya wazalishaji wa nguzo za umeme nchini, walioshiriki kikao baina yao na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (hayupo pichani), wakifuatilia kikao hicho kilichofanyika Makao Makuu ya Wizara, mjini Dodoma, Julai 24 mwaka huu.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mkuu wa Ujumbe wa Wazalishaji wa nguzo za umeme nchini, ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa AF, Severin Kalonga aliishukuru Serikali kwa kuwaamini na kuwapa nafasi ya kuzalisha nguzo hizo kwa matumizi yote ya hapa nchini.

Aidha, Kalonga aliahidi kuwa yeye na wenzake wamejipanga kutimiza malengo yote waliyopewa na Serikali katika kuhakikisha wanazalisha nguzo bora na zitakazotosheleza mahitaji ya nchi.

Kikao hicho baina ya wazalishaji wa nguzo za umeme nchini na Naibu Katibu Mkuu, kililenga kujadiliana kuhusu changamoto mbalimbali katika shughuli hiyo pamoja na kukubaliana namna ya kuzitatua baina ya pande hizo mbili kwa lengo la kuwezesha ufanisi unaotarajiwa katika eneo husika.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@mem.go.tz,                                             

Tovuti: mem.go.tz