EWURA yatathmini Bandari ya Mtwara kupokea mafuta kwa BPS

 

Na Wilfred Mwakalosi

EWURA inaangalia uwezekano wa kuifanya Bandari ya Mtwara kupokea shehena za mafuta kupitia mfumo wa uagizaji Mafuta kwa Pamoja (BPS).

Ikifanikiwa, mkoa wa Mtwara utakuwa wa tatu kupokea mafuta kupitia bandari zake, baada ya bandari za Dar es Salaam na Tanga. Tanzania inaagiza mafuta kupitia mfumo wa uagizaji wa pamoja, na shehena zote za mafuta zinapitia kwa sasa Dar es Salaam na Tanga tu.

Hivi karibuni timu ya wataalam wa EWURA ilitembelea bandari ya Mtwara kutathmini uwezekano wa kuitumia bandari hiyo kupokelea mafuta.

Timu hiyo ilikagua miundombinu ya kupokelea mafuta bandarini, pamoja na miundombinu ya kuhifadhia mafuta inayomilikiwa na kampuni za OilCom na GM Investment mkoani Mtwara.

Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bw. Felix Ngamlagosi alisema ni muhimu kwa mdhibiti kujionea mwenyewe hali ya miundombinu kabla ya kufanya lolote, ili kukuandaa mipango ya kuifanya Mtwara iweze kupokea shehena za mafuta.

Bw. Ngamlagosi alisema: “Tunafanya tathmini kujiridhisha juu ya mambo matatu: ukubwa wa soko la mafuta, miundombinu, na uwezo wa bandari kupokea shehena za mafuta. Tayari tunashirikiana na Uongozi wa Mkoa, TPA, TRA na kampuni za mafuta. Tunatarajia ushirikiano mkubwa toka kwao. Ni wadau wetu muhimu.”

Wachambuzi wa uchumi wanasema itakuwa nafuu Zaidi kiuchumi iwapo Bandari ya Mtwara itaweza kutumika kusaifirishia hata shehena za nchi jirani, kwa sababu hakuna foleni kama ilivyo kipande cha kilomita 100 kati ya Dar es Salaam na Chalinze, ambapo malori yanapoteza masaa kadhaa.

“Shehena inaweza kusafirishwa kutoka Mtwara hadi Zambia au nchi yoyote jirani kwa muda mfupi Zaidi ukilinganisha na njia ya Dar es Salaam,” mchambuzi mmoja alisema.

Bw. Ngamlagosi alisema mfumo wa BPS ambao ulianza mapema mwaka 2012, umekuwa wa manufaa makubwa  kwa taifa, ambayo ni pamoja na kupungua kwa bei za mafuta, utii wa sharia na kanuni, uwazi, usahihi wa takwimu na uepukaji wa uchelweshaji shehena bandarini unaotokana na msongamano wa meli.
Mkurugenzi Mkuu alisema mfumo wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja umeisaidia sana nchi, na kwamba umeokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kugharamia malipo ya uchcleweshaji meli bandarini.
“Toka kuanza kwa mfumo huu, uchakachuaji, ambalo lilikuwa tatizo sugu kwa miaka mingi, limepungua kwa kiwango kikubwa sana,” Bw. Ngamlagosi alisema.
Mfumo huu ulianzishwa ili kuhakikisha nchi inapata mafuta kwa gharama zinazotokana na ushindani ili kupata unafuu, kwa kununua kutoka kwa waagizaji walioshindanishwa na kuchaguliwa, kupitia zabuni za za kimataifa ili kupata unafuu wa kiuchumi.

Utafiti uliofanywa miaka ya karibuni na Chuo kikuu cha Dar es Salaam, idara ya Uchumi, umebaini kwamba  manufaa ya kifedha yanayotokana na hatua za kiudhibiti za EWURA kwenye eneo la bidhaa za petroli, yamethibitisha kwamba mfumo wa BPS umepunguza sana bei za mafuta, na kuleta uwazi kwenye biashara.