Home » images »

Hafla ya uzinduzi usanifu wa awali mradi wa bomba la mafuta yafanyika Uganda

 

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo tarehe 9/1/2017 aliongoza Ujumbe wa Tanzania jijini Kampala nchini Uganda katika hafla ya Uzinduzi wa Usanifu wa Awali (Front End Engineering Design -FEED) wa mradi wa Bomba la kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga, Tanzania.

Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospter Muhongo (wa tatu kushoto) na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda Mhandisi Irene Muloni (wanne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Hafla ya Uzinduzi wa Usanifu wa Awali wa michoro ya mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda Hadi Bandari ya Tanga Tanzania mjini Kampala Uganda.

Uzinduzi huo ulifanyika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini ya Uganda na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri wa nchi zote mbili za Uganda na Tanzania, Makatibu Wakuu wa nchi zote mbili, Wakurugenzi wa mashirika ya mafuta na gesi, Kampuni zilizogundua mafuta nchini Uganda za Total (Ufaransa), CNOOC (China), TULLOW (Uingereza), Kampuni ya Mafuta ya Uganda National Oil Co. (UNOC), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na wawakilishi wa vyombo vya habari.

Wakati wa uzinduzi huo ilielezwa   kuwa, FEED ni moja ya hatua muhimu katika kuhakikisha mradi huo unatekelezwa katika viwango vinavyozingatia usalama wa kimazingira na ustawi wa jamii.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo akisaini kitabu cha Wageni katika Ubalozi wa Tanzania nchini Uganda baada ya kuhudhuria Hafla ya Uzinduzi wa Usanifu wa Awali wa Michoro ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga, Tanzania. Wengine wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Kapuulya Musomba na Mtaalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Marwa Petro.

Vilevile, ilielezwa kuwa, hatua hiyo itajumuisha pia upatikanaji wa njia ya gharama nafuu ya kupitisha bomba la mafuta ambapo pia Wataalamu wa taaluma mbalimbali watahusika katika kuhakikisha mradi huo unafuata viwango na ubora wa kimataifa.

Pia , imeelezwa  kuwa bomba hilo litakuwa la kwanza kwa urefu duniani kuwa bomba linalopashwa joto muda wote kutokana na asili ya mafuta yanayosafirishwa.

Mradi huo mkubwa utatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali za Uganda na Tanzania na pia utahusisha kampuni za TOTAL, CNOOC na TULLOW.

Imeandaliwa na:

Asteria Muhozya,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz