Home » images »

Hivi ndivyo wasemavyo viongozi Shinyanga kuhusu REA III

 

Hivi karibuni, Aprili 2 2017, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, alizindua Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kwa Mkoa wa Shinyanga.

Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), Mkoa wa Shinyanga.

Uzinduzi huo uliofanyika katika Kijiji cha Negezi, Wilaya ya Kishapu mkoani humo, ulihudhuriwa na wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na wawakilishi wa wananchi.

Miongoni mwa Viongozi walioshiriki Hafla hiyo ya Uzinduzi ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba, Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga ambaye ni Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), Mkoa wa Shinyanga.

Viongozi hao walipata fursa ya kuzungumza katika Hafla husika na haya ndiyo waliyosema:

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga/Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba

 • Kwa niaba ya wananchi wa Shinyanga, natoa shukrani za dhati kwa Serikali kwa kuikumbuka Shinyanga. Tuna faraja kubwa kuwa ifikapo 2021, Mkoa mzima utakuwa umepata umeme.
 • Mradi umetupa matumaini kwani tunaamini uwepo wa umeme utachochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
 • Serikali ya Awamu ya Tano ni ya Viwanda. Umeme utatusaidia kuanzisha viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa, hivyo kurahisisha upatikanaji wa ajira. Aidha, utatusaidia kupunguza uharibifu wa mazingira ikiwemo kukata miti kwa ajili ya matumizi ya kupikia.
 • Hii ni fursa kubwa na tunaahidi kuitumia vizuri. Tutatoa ushirikiano kwa wakandarasi watakaokuwa wakitekeleza Mradi huu na tutahakikisha tunakuwa nao bega kwa bega mpaka Mradi utakapokamilika.

  Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga ambaye ni Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), Mkoa wa Shinyanga.

Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga na Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige

 • Shukrani kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa na nzuri anayofanya kwa wananchi wa Tanzania kwenye maeneo mbalimbali ya maendeleo.
 • Wakati wa Kampeni za uchaguzi mwaka 2016 tuliahidi ahadi mbalimbali kwa wananchi, ikiwemo ya kusambaza umeme kwenye vijiji vyote. Niombe kufikishiwa salamu za pekee kwa Mheshimiwa Rais, kwani kabla ya miezi 24 kutimia tangu alipoingia madarakani, leo Shinyanga tunazindua Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye Vijiji vyote. Wana Shinyanga tunamshukuru sana.
 • Nawashukuru Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Naibu Waziri, Dkt Medard Kalemani kwa uchapakazi wenu. Ninyi ni wapenzi wa watanzania, ni marafiki wa wana-Shinyanga. Asanteni kwa kuifanya Shinyanga ing’are.
 • Ninaomba, pamoja na kuwepo Mkandarasi mkubwa atakayesambaza umeme, wawepo pia wakandarasi wadogo wadogo ili kuharakisha kazi, iweze kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi

 • Jimbo la Kishapu ni miongoni mwa majimbo yaliyonufaika na miradi ya umeme kuliko jimbo linguine lolote katika nchi hii. Tulibahatika kupata Mradi mkubwa wa umeme wa kutoka Nyasamba mpaka Kata ya Songwa ambao umeunganishwa vijiji vingi sana.
 • TANESCO wametengeneza historia ya kuweka umeme hata katika nyumba za tembe.
 • Tunaomba mumpelekee salamu Mheshimiwa Rais na mumweleze kuwa wana-Kishapu wanayo furaha sana kwa miradi mikubwa ya umeme ambayo imefika hadi katika vijiji ambavyo hatukuwahi kutegemea.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

BaruaPepe: info@mem.go.tz                                             

Tovuti: mem.go.tz