Hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini Mh. Sospeter Muhongo akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2016/17

 

           UTANGULIZI

  1. Mheshimiwa Spika,   naomba   kutoa   Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka 2015/16 na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini pamoja na Taasisi zake kwa Mwaka 2016/17.
  2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuniwezesha kuwasilisha Hotuba hii kwa mara ya kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Uchaguzi huo uliwezesha Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Tano kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). Nampongeza kwa ushindi huo uliodhihirisha kukubalika kwake kwa Watanzania, hususan kutokana na uchapakazi na ufuatiliaji wake wa masuala ya maendeleo. Ni ukweli usiopingika kwamba maamuzi anayoyachukua na mbinu anazozitumia katika kuongoza Taifa letu ni za kipekee na zinatakiwa kuungwa mkono na kila Mtanzania bila kujali tofauti ya itikadi zetu.
  3. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nampongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa kwake kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuandika historia mpya ya nchi yetu ya kuwa Mwanamke wa Kwanza kushika wadhifa huo. Hii ni ishara njema kwa nchi yetu katika kuongeza nafasi za juu za wanawake katika Uongozi wa Taifa letu.
  4. Mheshimiwa Spika, vilevile, natumia nafasi hii kumpongeza Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
  5. Mheshimiwa Spika, nakupongeza wewe binafsi Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, nimpongeze Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb.) kwa kuchaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge letu Tukufu.
  6. Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu kwa kuniteua kuongoza Wizara ya Nishati na Madini. Niwahakikishie Watanzania kwamba nitatumia weledi na uzoefu wangu wote katika kuhakikisha kuwa Sekta za Nishati na Madini zinaleta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa Taifa letu.
  7. Mheshimiwa Spika, nampongeza Mhe. Doto Mashaka Biteko (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mhe. Deogratias Francis Ngalawa (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo. Vilevile, nawashukuru wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa ushauri na maoni yao katika kuendeleza na kusimamia Sekta za Nishati na Madini. Aidha, nawapongeza Wenyeviti wa Bunge, Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuteuliwa kwao kuwawakilisha wananchi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

>>Soma Zaidi>>