Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2014/15

 

Hotuba ya Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Prof. Sospeter Mwijarubi Muhongo (Mb.), amewasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2014/15

A. UTANGULIZI

  1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka 2013/14 na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zilizo chini yake kwa Mwaka 2014/15.
  2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kutekeleza majukumu yangu kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.
  3. Mheshimiwa Spika, kipekee nawashukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.) kwa uongozi na juhudi zao katika kuleta maendeleo ya Taifa letu na kwa ushirikiano wanaonipa katika kusimamia na kutekeleza majukumu ya Wizara ya Nishati na Madini.
  4. Mheshimiwa Spika, naomba kumpongeza kwa dhati Rais wetu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kupewa Tuzo ya Utumishi Bora kwa kuwa Kiongozi mwenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Bara la Afrika kwa Mwaka 2013. Hii ni heshima kubwa na Tunu kwa Watanzania wote kwa ujumla kwa kuthaminiwa na kutambuliwa kwa kiongozi wetu katika medani za kimataifa. Tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu ili azidi kumpa nguvu na hekima zaidi ya kutekeleza majukumu yake.
  5. Mheshimiwa Spika, napenda pia kukupongeza wewe binafsi, Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge na Wenyeviti wote wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kuliongoza Bunge hili Tukufu kwa hekima, busara, umahiri na bila kuyumba katika kusimamia Kanuni tulizojiwekea sisi wenyewe. Vilevile, namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Victor Kilasile Mwambalaswa (Mb.), Makamu Mwenyekiti Mhe. Jerome Dismas Bwanausi (Mb.), na wajumbe wote wa Kamati hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuishauri na kuisimamia Wizara katika utekelezaji wa majukumu yake. Naipongeza Kamati hiyo kwa kuchambua na kupokea Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara kwa Mwaka 2013/14 na Makadirio ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka 2014/15. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ya Nishati na Madini itaendelea kupokea ushauri na mapendekezo ya Kamati hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa yamezingatiwa katika kuandaa Bajeti inayowasilishwa kwenu. >> soma zaidi >>