Home » images »

Kaya 1600 Njombe kupata umeme mwakani

 

Kaya 1600  katika vijiji kumi mkoani Njombe  zinatarajiwa kupata umeme wa uhakika mara baada ya kukamilika kwa mradi wa uzalishaji wa umeme kwa kutumia maporomoko ya maji wa Luponde Hydro Ltd unaotekelelezwa na kampuni ya  Rift Valley Energy.

Meneja Uendeshaji kutoka kampuni ya kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko madogo ya maji ya kampuni ya Rift Valley Energy, Joel Gomba (kulia) akielezea hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Luponde Hydro Ltd kwa mtaalam kutoka Sehemu ya Nishati Jadidifu, Wizara ya Nishati na Madini, Emillian Nyanda (kushoto) mkoani Njombe.

Hayo yalielezwa leo na Meneja Mradi  wa Luponde Hydro, Mugombe Maxwell katika ziara ya wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini katika mkoa wa Njombe ili kujionea maendeleo ya miradi midogo ya  umeme wa maporomoko ya maji na nishati  jadidifu inayotekelezwa katika mkoa huo.

Maxwell alisema kuwa kampuni ya Rift Valley Energy ina miradi miwili ambayo ni Mwenga Hydro Grid wenye uwezo wa Megawati 4.1na Luponde Hydro Ltd utakaokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 3 mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wake hivyo kuwezesha vijiji kumi katika mkoa huo kupata umeme wa uhakika ifikapo mwakani.

Sister Richardis Chiwinga kutoka katika mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Benedict Sisters of Saint Agnes Chipole (katikati) akielezea hali ya maji katika bwawa la mradi huo kwa wataalam wa nishati jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini.

Akielezea mradi huo wa Luponde Hydro Ltd, Maxwell alisema kuwa mradi ulianza mwaka 2016 na kuongeza kuwa mradi huo upo katika maeneo mawili ambayo ni Luhololo na Igola yote yakiwa mkoani Njombe.

Akielezea ujenzi wa mradi huo, Maxwell alieleza kuwa mradi  umegawanyika katika awamu mbili na kuendelea kusema kuwa awamu ya kwanza inahusisha usambazaji  wa umeme wa uhakika katika  vijiji saba vyenye kaya 1120, shule tisa na vituo vya afya vitano.

Meneja Uendeshaji kutoka kampuni ya kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko madogo ya maji ya kampuni ya Rift Valley Energy, Joel Gomba (kulia) akionesha sehemu ya kuchepushia maji katika mradi wa Luponde Hydro Ltd uliopo katika hatua ya ujenzi mkoani Njombe kwa mtaalam kutoka Sehemu ya Nishati Jadidifu, Wizara ya Nishati na Madini, Emillian Nyanda (kushoto).

Aliongeza kuwa, awamu ya pili inahusisha usambazaji wa umeme wa uhakika katika  vijiji vitatu vyenye kaya 180.

Akielezea  hatua iliyofikiwa ya  utekelezaji wa mradi huo, Maxwell alisema kazi katika eneo la  Luhololo imekamilika kwa asilimia 60 kwa kazi za kawaida na asilimia 40 katika ujenzi wa mitambo.

Sehemu ya bwala la maji katika mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maji wa Benedict Sisters of Saint Agnes Chipole, Mbinga mkoani Ruvuma.

Aliongeza kuwa katika eneo la Igola mradi umekamilika kwa asilimia 40 na kusisitiza kuwa kampuni itahakikisha kuwa ujenzi katika maeneo yote unakamilika ifikapo mwakani ili wananchi wapate umeme wa uhakika.

Alisisitiza kuwa lengo la mradi ni kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na umeme wa uhakika na kuchangia  ukuaji wa  uwekezaji kwenye  viwanda  hususan katika maeneo ya vijijini, hivyo kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.

Imeandaliwa na:

Greyson Mwase,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz