Home » images »

Kinyerezi II ikamilike Septemba, 2018-Dkt. Kalemani

 

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amewaagiza Watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa Mradi wa kuzalisha umeme wa kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi II (MW 240) uwe umekamilika ifikapo Septemba 2018 kwa kuwa hakutakuwa na nyongeza ya utekelezaji wa mradi husika.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani, akiwa katika ziara ya kutembelea mradi ya Umeme ya Kinyerezi I na II (mweye suti ya bluu). Wengine katika picha ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Dkt. Tito Mwinuka (wa kwanza kulia), Meneja Mradi wa Kinyerezi I na II, Mhandisi Simon Jilima (kushoto) na Meneja Mwandamizi Miradi wa TANESCO, Gregory Chegere (wa pili kulia).

Aliyasema hayo tarehe 30/06/2017 akiwa kwenye Ziara ya kukagua vituo vya umeme vya kinyerezi I na II, Mbagala na Kurasini.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, kati ya megawati hizo 240, megawati 30 zitaanza kuzalishwa Desemba 2017 na kuanzia Januari 2018, zitazalishwa megawati 30 kila mwezi hadi ifikapo Septemba 2018.

Aliagiza TANESCO na Mkandarasi ambaye ni kampuni ya SUMITOMO kuhakikisha kuwa wanafanya kazi usiku na mchana ili mradi ukamilike kama ilivyopangwa. “Wananchi wa Tanzania wanahitaji umeme na pia Serikali ya Tanzania inaongelea suala la ‘Tanzania ya viwanda’ hivyo ni lazima tuhakikishe kwamba tunaenda kwa kasi ili kutimiza malengo tuliyojiwekea.” Alisema Dkt.Kalemani.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kulia) akikagua maendeleo ya ujenzi wa vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia Gesi Asilia vya Kinyerezi 1 na II vilivyopo jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka, wa tatu kutoka kushoto, Meneja Mradi wa Kinyerezi I na II, Mhandisi Simon Jilima. Wengine ni wawakilishi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO.

Aliongeza kuwa, Serikali imepanga kuzalisha megawati 5000 ifikapo 2020 ili kuweza kuwa na umeme mwingi na wa uhakika utakaoendesha viwanda husika.

Vile vile aliwaagiza Watendaji wa TANESCO kuhakiksha kuwa kazi ya upanuzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi I (Megawati 185) inayofanywa na kampuni Jacobsen Elektro ya Norway inakamilika pia Agosti 2018 na hivyo kufanya mradi huo wa Kinyerezi I uzalishe jumla ya megawati 335.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Kinyerezi I na II, Mhandisi Simon Jilima, alisema kuwa watazingatia maagizo ya Naibu Waziri ya kukamilisha miradi husika ndani ya wakati ulioagizwa.

Imeandaliwa na:

Rhoda James,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@mem.go.tz,                                                                               

Tovuti: mem.go.tz