Magufuli, Museveni wasaini tamko la pamoja mradi wa bomba la mafuta

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni mapema leo Mei 21, 2017  wametia  saini  tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano ya vipengele vya mkataba ambao utasainiwa baadaye kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania.

Hafla hiyo  iliyofanyika  Ikulu jijini Dar es Salaam  ilihudhuriwa pia na  viongozi mbalimbali wa nchi zote mbili wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wanasheria Wakuu wa Serikali, Wakurugenzi na Viongozi wa Taasisi mbalimbali zinazohusika na mradi huo.

Baada ya utiaji saini wa tamko  hilo, wataalam wataandaa mkataba wa mradi kati ya Tanzania na Uganda ambao umepangwa kukamilika ndani ya kipindi cha wiki moja, na baada ya hapo  taratibu za kuweka jiwe la msingi  la kuanza kwa ujenzi wa mradi huo  zitafanyika.

Mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo wenye urefu wa jumla  ya Kilometa 1,443 zikiwemo  1,115 zitakazojengwa katika ardhi ya Tanzania utakaogharimu jumla ya Dola za Marekani Bilioni 3.55, unatarajiwa kusafirisha mapipa laki mbili na kutoa ajira kati ya 6,000 na 10,000.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa utiaji  saini  wa tamko  hilo, Rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. John Pombe Magufuli, alisema kukamilika kwa mradi huo kutaleta mabadiliko  ya kiuchumi katika nchi  za Uganda na Tanzania.

Akielezea mradi huo, Dkt Magufuli alisema kuwa mradi ulikuwa na ushindani mkubwa hata hivyo bado ilionekana Tanzania kuwa na vigezo vya bomba hilo kupita katika sehemu kubwa ya ardhi yake ambapo alieleza vigezo hivyo kuwa ni pamoja na hali ya tambarare katika ardhi ya Tanzania hivyo gharama za uwekezaji kuwa rahisi.

Aliongeza kuwa ardhi ya Tanzania ni rahisi pamoja na kuwepo kwa hifadhi ya barabara katika maeneo mengi hali inayopelekea gharama za fidia kuwa ndogo

Rais Magufuli aliendelea kueleza vigezo vingine kuwa ni pamoja na Tanzania kuwa na uzoefu mkubwa katika usimamizi wa bomba la mafuta na gesi kama vile bomba la mafuta la TAZAMA na la gesi linalotoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam.

“Pia bandari ya Tanga ni nzuri kwa kuwezesha mafuta kusafirishwa kwa mwaka mzima bila tatizo lolote,” alisema Rais Magufuli.

Akielezea manufaa yatakayopatikana mara baada ya kukamilika kwa mradi huo Rais Magufuli alisema nchi za Tanzania na Uganda zitapata mapato na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wake

Alieleza faida nyingine ni pamoja na gharama za mafuta kupungua kutokana na nchi za Afrika Mashariki kutumia mafuta yake yenyewe kwenye magari pamoja na ndege hivyo kuchochea kasi ya utalii katika nchi husika pamoja na ajira.

Dkt. Magufuli aliwataka wataalam kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi ili uweze kukamilika kwa wakati na wananchi wa nchi zote mbili kuanza kufaidi matunda ya mradi huo.

Naye Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alimpongeza Rais Magufuli na  Serikali yake kwa kutia msukumo mkubwa kufanikisha mradi huu na kuongeza kuwa mradi utazinufaisha nchi za Afrika Mashariki yakiwemo mashirika  ya ndege ambapo yatapata mafuta kwa gharama nafuu na kukua zaidi kibiashara.

Imeandaliwa na:

Greyson Mwase,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@mem.go.tz,                                                                               

Tovuti: mem.go.tz