‘Makala’ Sera ya madini ni mkombozi wa wanawake wachimbaji?

 

“Mjomba Hussein” atoa ushahidi

Hivi karibuni, Wizara ya Nishati na Madini iliendesha mafunzo maalum kwa wachimbaji madini ambao miradi yao ilichaguliwa kupata ruzuku ya Serikali kwa ajili ya kuendeleza uchimbaji mdogo.

Miradi iliyochaguliwa kwa ajili ya kupata ruzuku ilikuwa ya aina mbalimbali na pia ilihusu jinsia zote. Miradi hiyo ni pamoja na ile ya uchimbaji madini, utoaji wa huduma za kiufundi, uchenjuaji madini, usanifu wa vito na pia huduma za mama lishe migodini.

Mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha wachimbaji madini wadogo nchini kuendeleza shughuli zao kwa tija na yalihitimishwa kwa utoaji mikataba ya wachimbaji madini wadogo waliopata ruzuku kutoka Serikalini awamu ya pili.

Mambo mbalimbali yalijadiliwa na washiriki wa mafunzo hayo ambapo baadhi ya washiriki waliipongeza Serikali kwa kuwashirikisha wanawake kwa upana zaidi katika uwezeshaji wa shughuli za uchimbaji mdogo.

Kufuatia pongezi hizo, nilitamani pia kupata mtazamo wa washiriki wa semina ikiwa Sera ya Madini ni Mkombozi wa Wanawake wachimbaji wa madini kwa kuwa kundi hili ni mhimili wa maendeleo ya jamii yoyote.

Katika kutafuta jibu la swali hilo, nilizungumza na wadau mbalimbali, na hususan wanawake wawili kutoka Merelani, waliojitambulisha kama Pili Hussein na Susie Kennedy.

Nilivutiwa kuzungumza kwa kirefu na Pili Hussein ambae ni mama wa makamo, na alikuwa na historia ya pekee katika uchimbaji wa madini ya Tanzanite tokea mwaka 1988 katika eneo la Merelani, Mkoani Manyara.

Pili anasema wakati akianza shughuli za uchimbaji, jamii kwa wakati huo iliichukulia shughuli hiyo kuwa ya wanaume pekee hivyo yeye alilazimika kujificha kwa kivuli cha mwanaume akitumia jina la bandia la ‘Mjomba Hussein’.

“Nililazimika kuiaminisha jamii iliyonizunguka katika kazi zangu kuwa mimi ni mwanaume na siyo mwanamke ili niweze kukubalika kufanya kazi hiyo,” anasema mama huyo.

Anasema alilazimika kuchanganyika na wanaume katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuvaa mavazi ya kiume muda wote, kuvuta sigara, na mambo mengine kadhaa ambayo kwa wakati huo ilikuwa aghalabu kwa mwanamke kufanya. “Hata jina la Mjomba Hussein lilianza wakati huo,” anasema Pili.

Pili au ‘Mjomba Hussein’, anawakilisha wanawake katika jamii yetu ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikatishwa tamaa kutokana na mitazamo hasi ya baadhi ya watu hivyo kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo kwa dhana kuwa kazi hizo zinafaa kufanywa na wanaume tu.

Aidha, kutokana na Sera za miaka ya nyuma, hasa wakati wa ukoloni kutotambua rasmi uchimbaji mdogo, suala la ubaguzi wa jinsia lilikuwa na nguvu zaidi kwa kuwa uchimbaji ambao ulionekana kuwa haramu ulihitaji wanaume wenye kuweza kupambana na Serikali ilipobidi.

Ni jambo la kutia faraja kuwa Serikali imekuwa ikipambana na mitazamo na dhana hizo potofu zilizojengeka kwa muda mrefu katika jamii yetu kwa kuwajengea mazingira wezeshi wanawake ili waweze kufanya kazi mbalimbali za kujiletea maendeleo pasipo kuwa na hofu ya aina yoyote.

Wizara ya Nishati na Madini mathalani, imekuwa ikifanya jitihada za kuwawezesha wanawake kushiriki katika shughuli mbalimbali zinazohusu sekta husika ikiwa ni pamoja na uchimbaji mdogo wa madini.

Katika awamu hii ya pili ya utoaji ruzuku, Serikali imepanua zaidi wigo ambapo imetenga takribani Shilingi za Kitanzania bilioni 7.2 kwa vikundi 111 vya wachimbaji wadogo na watoa huduma mbalimbali katika sekta ya uchimbaji madini mdogo ukilinganisha na Dola za Marekani 500,000 sawa na takribani Shilingi za Kitanzania bilioni moja zilizotolewa kwa waombaji 11 katika awamu ya kwanza.

Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi wa Madini, Sehemu ya Leseni, Mhandisi John Nayopa, utoaji ruzuku katika awamu ya pili umehusisha wachimbaji wadogo pamoja na watoaji huduma mbalimbali katika sekta husika tofauti na ilivyokuwa katika awamu ya kwanza iliyofanyika katika Mwaka wa Fedha 2013/14 ambapo Wizara iliwalenga wachimbaji madini wadogo pekee.

Mhandisi Nayopa anafafanua zaidi kuwa, watoa huduma katika uchimbaji madini mdogo walionufaika na ruzuku awamu ya pili ni pamoja na vikundi vya wanawake wanaotoa huduma ya chakula, kushona nguo kwa wachimbaji madini na wale wanaojishughulisha na uongezaji thamani madini, hasa ukataji na uchongaji madini ya vito.

Aidha, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene wakati akifunga mafunzo kwa wachimbaji wadogo mjini Dodoma hivi karibuni aliwapongeza wachimbaji madini wanawake waliopata ruzuku awamu ya kwanza na kueleza kuwa wameonesha mfano mzuri kwa kutumia vizuri fedha walizopatiwa na hivyo kuongeza tija kwenye kazi zao.

Alitoa mfano wa mmoja wa walionufaika na awamu hiyo kuwa ni kampuni ijulikanayo kama Precision Décor inayomilikiwa na mwanamke na inajishughulisha na uchimbaji wa madini ya ujenzi yanayoitwa, Tanga stone.

Simbachawene aliwaasa wakina mama wachimbaji kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwa mfano wa kuigwa. “Natarajia pia katika awamu hii wanawake wataendelea kuwa mfano wa kuigwa. Dhana ya akina mama wakisaidiwa ni sawa na kusaidia jamii kubwa, inajitokeza hapa,” alisema Waziri.

Wakati huu ambapo Serikali imebainisha kwamba Wizara inaendelea kuweka mikakati mingi ili kuendeleza wachimbaji wadogo, ni fursa nzuri kwa wanawake kujitokeza kwa wingi na kufanya kazi za uchimbaji madini au utoaji huduma katika sekta husika ili waweze kunufaika ipasavyo.

Bila shaka Sera ya Madini ni mkombozi kwa wanawake hawa na wengine ambao watachangamkia fursa zilizopo kwenye sekta ya madini. Shime wanawake wachimbaji, tuendelee kuonyesha mfano kwa kuisaidia Serikali kutimiza azma ya kuhakikisha sekta ya madini inachangia kwa asilimia 10 katika Pato la Taifa ifikapo mwaka 2025.

Imeandaliwa na:
Veronica Simba,
Afisa Habari,
Wizara ya Nishati na Madini,
754/33 Mtaa wa Samora,
S.L.P 2000 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606
Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                                                                
Tovuti: mem.go.tz