Home » Latest »

Makala ya tetemeko la ardhi mkoani Kagera

 

Na Samwel Mtuwa

Taifa la Tanzania pamoja na nchi jirani ya Uganda  wataikumbuka siku ya tarehe 10 Septemba 2016 hasa katika majira ya mchana wa saa 9 na dakika 27 kutokana na tetemeko la  ardhi lilitokea katika mkoa wa Kagera na kupita katika mkoa wa jirani nchini Uganda , tetemeko hilo  likiwa na ukubwa wa kipimo cha  skeli  ya Richter 5.7.

Taarifa iliyotolewa na taasisi yenye dhamana ya kuchunguza majanga ya asili ijulikanayo kwa jina la Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) imeeleza kuwa  kitovu cha tetemeko hilo ni katika makutano ya latitude 1  06 na longitude 31 55 ikiwa ni umbali wa kilomita 20 kaskazini mwa kijiji cha Nsunga na kilomita  42 kaskazini magharibi mwa mji wa Bukoba, katika umbali wa kilomita 10 kutoka chini ya ardhi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa sababu ya tetemeko hilo ni misuguano ya mapange makubwa ya ardhi yaliyopasuliwa na mipasuko ya ardhi kwenye bonde la ufa  karibu na mkondo wa magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki.

Utafiti wa wanasayansi ya Jiolojia kupitia kitabu cha dunia kijulikanacho kama The World Book Encyclopedia wamesema kwamba tetemeko la ardhi ni mojawapo  ya matukio yenye kusababisha  uharibifu mkubwa kutokana na nishati  kubwa ya tetemeko la ardhi inayoweza kujitengeneza na kufikia ukubwa wa mara 10,000 zaidi ya  ile ya bomu la kwanza la nyuklia, watalaam wanasema hali hii ni ya kuogopesha kwa sababu inaweza kutokea katika tabia yoyote ya nchi , msimu wowote na saa zozote , na kwa kawaida wanasayansi wanaweza kujua kwa kadiri fulani mahala ambapo tetemeko lenye nguvu litatokea , ila hawawezi kutabiri litatokea lini.

Kwa mujibu wa taarifa za kituo kinachoshughulikia matetemeko ya ardhi nchini Marekani (NEIC) chini ya taasisi ya Jiolojia ya Marekani (USGS) inasema  tetemeko la ardhi hutokea  kwa sababu ya kusonga kwa miamba mikubwa ambayo iko chini ya uso wa dunia miamba hiyo husonga daima kidogo kidogo.

Mawimbi ya tetemeko la ardhi ambayo hutokea huwa dhaifu sana hivyo hayawezi kutambulia waziwazi katika uso wa dunia , ila yanaweza kutambuliwa na kurekodiwa na kifaa maalum yaani kipima tetemeko mapema pale  miamba inapovunjika na kusongasonga au kugonga kiasi cha kutetemesha ardhi kwa mawimbi makubwa katika uso wa dunia .

Kutokana na sababu hiyo tunaweza kujiuliza kuwa ni kwanini miamba hiyo huendelea kusongasonga? Taarifa za kitaalamu na utafiti zinasema kuwa ,jibu la msingi laweza kupatikana katika ile dhana kuhusu mabamba yaliyo kwenye tabaka la nje la dunia , dhana hii imepelekea kubadili kabisa maoni ya wanasayansi kuhusu dunia.

Kutokana na maoni hayo ya wanasayansi , uchunguzi umeonyesha kwamba kuna mabamba saba  makubwa yaliyo kwenye tabaka la nje la dunia ambayo yamegawanyika katika mabamba madogo madogo , utafiti umegundua  mabamba hayo husonga daima na kwa wakati mmoja kwa umbali wa kilomita 10 hadi 30 kila mwaka.

Kituo cha NEIC kinasema kuwa matetemeko mengi ya ardhi hutokea kwenye maeneo membamba ambako mabamba hayo yametengana, utafiti unaonyesha kuwa asilimia 90 ya matetemeko makubwa ya ardhi hutokea katika maeneo hayo.

Sababu nyingine inayotajwa na wanasayansi ni kuwa tetemeko la ardhi ni miendo ya vipande vinavyofanya sehemu ya nje ya dunia  kufanana kiasi cha chungwa yaani nje kuna ganda imara linaloitwa ganda la dunia na ndani yake sehemu kubwa ni giligili ya moto , hilo ganda la nje si kipande kimoja ila ni vipande mbalimbali vinavyoelea juu ya giligili moto ndani ya dunia.

Vipande hivyo kwa lugha ya kitaalamu huweza kuitwa mabamba ya ganda  la dunia , wakati vipande hivi vinasuguana na kusukumana  kunatokea msuguano na kushikana au kuachana kwa mabamba hayo na kusababisha  mishtuko ya tetemeko la ardhi.

Kitaalamu tetemeko la ardhi linaweza kupimwa kulingana na ukubwa au kiwango chake, kwa mfano katika miaka ya 1930 Charles Ritcher alibuni kipimo cha kuonyesha ukubwa wa matetemeko ya ardhi kijulikanacha kwa jina la “ Ritcher skeli”, vituo vya kupima  matetemeko ya ardhi vilipoanza kuongezeka  , vipimo vipya vilibuniwa kwa kutumia  uvumbuzi wa kipimo cha Richter, kwa kawaida kipimo cha  nguvu za tetemeko la ardhi huonyesha kiasi cha nishati inayotokezwa kwenye chanzo cha tetemeko la ardhi.

Nyakati nyingine vipimo hivyo havilingani na uharibifu uliosababishwa na tetemeko la ardhi kwa mfano tetemeko la ardhi lililotokea  kaskazini mwa Bolivia  mnamo mwezi Juni 1994 , tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa 8.2 kwenye kipimo cha Richter na ililipotiwa kuwa watu watano tu walipoteza maisha  lakini tofauti imeonekana katika tetemeko lilitokea Septemba 10, 2016 mkoani Kagera nchini Tanzania  lililokuwa na ukubwa wa kipimo cha Richter Skeli ya 5.7 lakini zaidi ya watu 10 walipoteza maisha pamoja na uharibifu wa miundombinu na makazi ya watu.

Sambamba na tofauti ya kipimo cha ukubwa, kiwango cha tetemeko la ardhi huonyesha jinsi linavyoathiri watu, majengo na mazingira , kiwango cha tetemeko la ardhi huonyesha waziwazi hasa jinsi wanadamu wanavyoathiriwa nalo.

Siku zote matetemeko ya ardhi hayajeruhi watu moja kwa moja bali majeruhi na vifo husababishwa na kuta zinazoanguka , mabomba ya gesi yaliyopasuka , nyaya na nguzo za umeme zilizokatika, miti na mawe yaliyoporomoka.

Watalaam wa sayansi ya miamba (Jiolojia) hupima tetemeko kwa njia mbalimbali kwa mfano kuna kipimo cha skeli mbili lakini zinazotumiwa mara nyingi ni ile ya Richter na Mercali, katika miaka ya nyuma skeli mpya ilianza kutumiwa kimataifa iliyojulikna kwa jina la “Moment Magnitude Scale (MMS)” skeli hii ina kiasi cha nguvu inayofanana zaidi na skeli ya Richter lakini iko makini zaidi kwa kutofautisha matetemeko makubwa.

Kipima tetemeko ni chombo kinachopima na kurekodi mtikisiko wa ardhi wakati wa tetemeko la ardhi linapotokea , kipima tetemeko cha kwanza kilibuniwa mwaka 1890, mpaka sasa kuna vituo zaidi ya 4000 ulimwenguni pote vinavyopima matetemeko ya radhi, Tanzania ikiwa na vituo tisa vya kupima matetemeko ya ardhi.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na GST juu ya tetemeko la kagera inasema mpaka sasa duniani kote hakuna teknolojia ,vifaa au taratibu za kuweza kutabiri utokeaji wa tetemeko la ardhi , teknolojia au vifaa vyote , taratibu au upimaji wa tetemeko la ardhi hutumika kupima ukubwa na tabia ya tetemeko baada ya kutokea.

Kwa upande mwingine Mhadhiri msaidizi wa chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM) Bi Eva Shayo aliutaarifu umma kuwa Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM) kwa kushirikiana na Taasisi ya mafunzo ya teknolojia Dar es salaam (DIT) wamefanikiwa kutengeneza mfumo wa kutabiri matetemeko ya ardhi yanayotokea nchini.

Akiongea na vyombo vya habari Mhadhiri alifafanua kuwa mfumo huo ulianza mwaka 2005 na unafanya kazi ya kutoa taarifa za awali juu tetemeko la ardhi hasa katika mikoa iliyopitiwa na bonde la ufa akitolea mfano mkoa wa Rukwa ,Mbeya ,Arusha, Ruvuma n.k.

Nchini Marekani kituo kikuu cha kuchunguza matetemeko cha NEIC kilicho chini ya taasisis ya USGS kupitia mpango maalum ulioitwa jina la sayansi ya kubadili dunia unaandaa program maalum ya kuchunguza, kutafiti, na kutoa ripoti au taarifa ya matetemeko itakayotumia mfumo wa hali ya juu ya kuchunguza matetemeko ya ardhi.

Ripoti ya mwaka 2015 ya Shirika la habari la kituo cha televisheni cha CNN ulipongeza juu ya program maalum  ya kompyuta ya kuchunguza matetemeko inayoandaliwa na NEIC imesema kwamba kukamilika kwa programu hiyo kutawasaidia watalaam wa sayansi  ya miamba (Jioloji) kuweza  kutambua mara moja mahala ambapo mtikisiko mkubwa  wa tetemeko la ardhi ulipotokea na mamlaka husika kuweza kutuma msaada  kwenye maeneo yaliyokumbwa na tetemeko.

Duniani kote inafahamika kuwa lengo kuu la watalaamu wa sayansi ya miamba juu ya matetemeko ni kutoa maonyo kuhusu matetemeko ya ardhi pamoja kutoa elimu juu ya njia stahiki za kujikinga na janga hilo la matetemeko ya ardhi.

 

Mwandishi wa makala haya ni Afisa Habari wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ,anapatikana kupitia namba ya simu 0756638393 , au barua pepe , mtuwasamwel@hotmail.com