Home » images »

Mkutano wa kimataifa wa udhibiti uvunaji haramu wa madini Tanzania wafanyika

 

Tanzania imekuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika. Mkutano ulifunguliwa na Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Prof.James Mdoe.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe (katikati, waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa ICGLR, Paul Ndarihonyoye na kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa ICGLR, Zachary Muburi-Muita.

Mkutano huo uliofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 25-27 Julai  2017,  umehudhuriwa na nchi wanachama 12 ambazo ni Tanzania, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda, Zambia, Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan  na Kenya.

Prof. James Mdoe, alisema kuwa, baadhi ya masuala muhimu yaliyojadiliwa katika Mkutano huo ni pamoja na matumizi ya hati moja ya usafirishaji madini, kuwianisha sheria za nchi wanachama ili kuwa na uwiano katika hatua za kudhibiti utoroshaji madini, pamoja na urasimishaji wa shughuli za wachimbaji wadogo.

Katibu Mtendaji wa ICGLR, Zachary Muburi-Muita akizungumza wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika, wa kwanza kulia ni Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe na katikati ni Mratibu wa ICGLR nchini Tanzania, Ali Musa.

Masuala mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na uongezaji wa ushiriki wa wanawake katika shughuli za uchimbaji madini, uwazi na uwajibikaji katika tasnia ya uziduaji (EITI)  pamoja na uzuiaji wa watoto katika shughuli za uchimbaji madini.

Alisema kuwa, pamoja na kujadili utekelezaji wa malengo  mbalimbali ya kamati hiyo na kupeana uzoefu wa shughuli za udhibiti wa uvunaji wa haramu wa madini katika nchi hizo, ICGLR itatoka na maazimio yanayopaswa kutekelezwa na nchi wanachama ili lengo la udhibiti wa uvunaji  haramu wa madini lifanikiwe.

Alisema kuwa, ICGLR inahusika na kuweka mfumo wa usimamizi katika shughuli za uchimbaji madini, uchenjuaji, usafirishaji na uuzaji wa madini ili kuhakikisha kuwa shughuli hizo zinafanywa kihalali na hazitumiwi na vikundi au watu wanaohusika katika kuendeleza migogoro na vita.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika unaofanyika jijini Arusha.

Kuhusu utekelezaji wa malengo ya ICGLR, Prof Mdoe alisema kuwa kwa upande wa urasimishaji wa shughuli za uchimbaji mdogo wa madini, Tanzania imeshatoa leseni za madini takriban 35,000 kwa watanzania ambapo asilimia kubwa ya leseni hizo zimetolewa kwa wachimbaji wadogo.

Alisema kuwa Tanzania pia inaboresha shughuli za uchimbaji mdogo wa madini kwa kutenga maeneo ya uchimbaji madini ambapo mpaka sasa Serikali imetenga eneo la kilometa za mraba 2000 kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini.

Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe (katikati,) akiwa na Wajumbe wa Mkutano wa Kimataifa wa 15 wa Kamati ya ICGLR ambayo inahusika na mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa madini katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu barani Afrika.

Aliongeza kuwa, huduma  kwa wachimbaji madini zimesogezwa hadi katika ngazi ya mikoa ambapo Ofisi hizo za madini zipo karibu na maeneo zinakofanyika shughuli za wachimbaji wadogo.

Kuhusu suala la uvunaji haramu wa madini pamoja usafirishaji wake, Prof. Mdoe alisema kuwa Tanzania inaungana na nchi wanachama wa ICGLR ili kuhakikisha kuwa malengo yanayowekwa na Kamati husika ya kudhibiti uvunaji haramu wa rasilimali yanatekelezwa ili rasilimali hizo zisitumike kwa matumizi haramu kama ya uchocheaji wa vita katika nchi wanachama.

Nao,  Mwenyekiti na Katibu Mtendaji wa kamati ya ICGLR, kwa nyakati tofauti waliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kukubali Mkutano huo muhimu kufanyika nchini Tanzania lengo likiwa ni kufanikisha utekelezaji wa mipango mbalimbali iliyowekwa na Kamati hiyo.

Walieleza kuwa, dhumuni la ICGLR ni kuhakikisha kuwa  Azimio la mwaka 2010 lililosainiwa na nchi za Maziwa Makuu kuhusu Itifaki ya mapambano dhidi ya uvunaji haramu wa rasilimali linatimizwa.

Imeandaliwa na:

Teresia Mhagama,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@mem.go.tz,                                                                               

Tovuti: mem.go.tz