Home » images »

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Kamati ya ulinzi watemebelea eneo la mradi wa bomba Chongoleani

 

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela na Uongozi wa Mkoa ikiwemo Kamati ya Ulinzi na Usalama tarehe 5 Aprili, 2017, walitembelea Chongoleani eneo itakapojengwa gati ya kupakua mafuta ya Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kuona maendeleo ya shughuli za mradi zinavyotekelezwa katika eneo hilo, lililopo nje kidogo ya Jiji la Tanga.

Akiwa katika eneo hilo, Shigela alipokea taarifa ya maendeleo ya mradi husika kutoka kwa Maafisa kuhusu maendeleo ya mradi huo.

Akitoa taarifa ya mradi kuhusu zoezi la utafiti kwa upande wa nchi kavu na baharini, Mtaalam wa Maji (Hydrologist) kutoka   Kitengo cha Mazingira, Wizara ya Nishati na Madini,  Mhandisi Alphonce Kilovele alisema kuwa, sampuli za udongo na maji zimekwisha patikana na zipo kwenye taratibu za kupelekwa maabara za ndani na nje ya nchi   kwa ajili ya uchunguzi wa takwimu mbalimbali za kihandisi.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga (katikati), Martine Shigela, akimsikiliza Mtaalam wa Maji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Alphonce Kilovele (watatu kushoto) baada ya kutembelea eneo la Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi, Chongoleani, Tanga itakapojengwa gati ya kupakua mafuta.

“ Tayari maeneo 6 yalishachorongwa visima vya sampuli za udongo katika Awamu ya kwanza. Eneo moja lililobaki litaendelea Awamu ya pili inayotarajiwa kuanza katikati ya mwezi wa nne,” alisema Kilovele.

Aidha, kwa upande wa utafiti wa Geophysics, Kilovele alisema kuwa, kwa sasa kuna mazoezi matatu (3) yanayoendelea ambayo kitaalamu yanajulikana kama, Seismic, Electrical na Microgravimetry.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa alipongeza hatua zilizofikiwa kuhusu mradi husika na hivyo kutumia fursa hiyo kuwaomba wananchi wa eneo hilo kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea na taratibu za uthamini na masuala mengine ya fidia.

“ Sheria zinazingatiwa, hivyo basi haki za wananchi zipo palepale. Endeleeni kushirikiana vizuri na viongozi wa mradi ili kuweza kukamilisha tafiti hizo ambazo zitasaidia kazi za usanifu wa mradi,” alisema Shigela.

Mbali na Kamati ya Ulinzi, wengine walioshiriki katika ziara hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Maafisa Tarafa, Viongozi wa Serikali ya Kata na Serikali za Mitaa ya Chongoleani na Putini.

Imeandaliwa na:

Asteria Muhozya,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz