Home » images »

Mpango kabambe wa kuendeleza sekta ndogo ya umeme 2016-40 wajadiliwa

 

Wadau mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali, Binafsi, na Wadau wa Maendeleo wamekutana jijini Dar es Salaam ili kujadili na kutoa mapendekezo yao katika Rasimu ya Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta Ndogo ya Umeme (PSMP) kwa mwaka 2016 – 2040.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa, Ntalikwa (katikati) akizungumza katika Warsha ya Wadau kujadili Mpango Kabambe wa Uendelezaji Sekta Ndogo ya Umeme nchini. Wengine katika picha ni Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akifungua Warsha hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa, alisema kuwa mapendekezo yaliyotolewa na Wadau hao yatasadia kuboresha Rasimu hiyo ambayo itakuwa ni muongozo katika upatikanaji na usambazaji wa Nishati ya Umeme wa uhakika nchini.

Alisema kuwa, Mpango huo ni muhimu kwa maendeleo ya Sekta ya Nishati kwani utaainisha  miradi ya umeme inayotakiwa kutekelezwa ili kutimiza mahitaji ya umeme ya muda mrefu, kati na mfupi ndani ya kipindi cha miaka 25 ijayo.

Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Toshio Nagase akizungumza katika Warsha ya Wadau kujadili Mpango Kabambe wa Uendelezaji Sekta Ndogo ya Umeme nchini. Wengine katika picha ni Watendaji kutoka JICA pamoja na Mshauri Mtaalam kutoka kampuni ya Yachiyo Engineering, Kyoji Fuji (wa kwanza kulia).

Profesa Ntalikwa alieleza kuwa kazi ya kuandaa Rasimu ya Mpango huo imetekelezwa na Kikosi Kazi cha Wataalam kutoka Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Mshauri Mtaalam aliyeajiriwa na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Alisema kuwa kabla ya kutoa maoni hayo,  Kikosi Kazi hicho pamoja na JICA kilishaainisha makadirio ya mahitaji ya umeme, kuainisha mipango ya uzalishaji na usafirishaji umeme  ili kukidhi mahitaji ya muda mfupi, kati na mrefu,   gharama za uwekezaji na athari  za kimazingira hivyo alitoa wito kwa Wadau hao kuwa huru katika kutoa maoni mbalimbali na kuhoji ili kuweza kuwa na PSMP bora.

Wadau mbalimbali wakiwa katika Warsha iliyolenga kujadili Mpango Kabambe wa Uendelezaji Sekta Ndogo ya Umeme nchini iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa JICA ndiyo ilifadhili  zoezi zima la uandaaji wa Mpango huo na kutumia fursa hiyo kulishukuru Shirika hilo kwa kukubali  kutoa  kiasi cha Dola za Marekani milioni 2.8 kwa ajili ya kazi husika.

Vilevile alisema kuwa,  Serikali ya Japan kupitia JICA imeongeza ufadhili wake katika miradi ya umeme kwa kiasi cha Yen 4.41 Bilioni sawa na Dola za Marekani milioni 38 ambapo miradi hiyo inajumuisha  uboreshaji wa miundombinu ya usambazaji umeme jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa JICA nchini, Toshio Nagase alisema kuwa, Serikali ya Japan imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika masuala ya kijamii na miradi ya maendeleo kwa muda wa miaka 50  na katika miradi ya Nishati imeendelea kufadhili miradi hiyo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kati ya Dodoma -Singida na Singida- Shinyanga.

Kamishna Msaidizi wa Nishati anayeshughulikia Umeme, Mhandisi, Innocent Luoga akizungumza katika Warsha ya Wadau kujadili Mpango Kabambe wa Uendelezaji Sekta Ndogo ya Umeme nchini. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa. Wa kwanza kushoto Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, na wa Pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Felchesmi Mramba.

Alisema kuwa, JICA pia imeshiriki katika kufadhili  uboreshaji  wa mifumo ya usambazaji umeme jijini Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar ambapo kiasi cha fedha walichotoa ni Yen milioni 200.

Kuhusu Mpango huo Kabambe wa Umeme,  Nagase alisema kuwa unaainisha mahitaji halisi ya umeme yenye kukidhi malengo ya Serikali ya kuongeza kiwango cha uzalishaji umeme kufikia Megawati 5,000 ifikapo mwaka 2020 na Megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

Alisema kuwa,  PSMP  pia inaainisha ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme wa msongo wa  kV 132 mpaka 400K kVambapo urefu wa miradi yote ya usafirishaji umeme inakadiriwa kuwa na umbali wa km 12,620 hadi kufikia mwaka 2040.

PSMP pia imeainisha gharama za uwekezaji kwa miradi yote ya uzalishaji na usafirishaji umeme hadi mwaka 2040 ambayo inakadiriwa kufikia Dola za Marekani Bilioni 49. 229.

Vilevile alisema kuwa PSMP ni muhimu kwani inaiwezesha pia Serikali kujua gharama halisi za uwekezaji katika Sekta ndogo ya Umeme ili kuweza kuchukua hatua stahiki za kuendeleza miradi iliyoainishwa ikiwemo utafutaji wa vyanzo vya fedha vya kuendeleza miradi husika.

Imeandaliwa na:

Teresia Mhagama na Nuru  Mwasampeta,

Maafisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                           

Tovuti: mem.go.tz