Home » images »

Mpango wa Nishati endelevu kwa wote (SE4ALL) kuanza kutekelezwa

 

Utekelezaji wa Mpango Endelevu wa miaka mitano 2017-2022 wa Nishati Endelevu kwa Wote (SE4All) unatarajiwa  kuanza hivi karibuni baada ya kamati inayohusika na mpango huo kukaa ili kujadili na kupitisha mikakati ya utekelezaji wa mpango huo.

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishaji Dkt. Mhandisi Juliana Palangyo (mwenye miwani mbele) akifuatiwa na Mshauri mwelekezi kutoka UNDP Dkt. Balasankari, B.E.M.Engg kushoto kwake mara baada ya kikao hicho kufungwa rasmi na Mhandisi Pallangyo.

Haya yamebainika tarehe 12 April, 2017 wakati kamati hiyo iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa nishati kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Taasisi za serikali, Mashirika binafsi na yale ya Umoja wa Mataifa  walipofanya kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya Taifa (BOT) jijini Dar es Salaam.

Akielezea juu ya utekelezaji wa programu hiyo Injinia Emillian Nyanda Mtaalamu kutoka sehemu ya Nishati Jadidifu Wizara ya Nishati na Madini, alisema kuwa programu hiyo itatekelezwa ndani ya miaka mitano ikiwa ni jitihada za Umoja wa Mataifa za kufikisha huduma ya nishati kwa wote ili kuongeza kiwango cha maendeleo kwa wananchi.

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishaji Dkt. Mhandisi Juliana Palangyo (katikati) akiwa katika picha na Katrine Vestbostad kutoka ubalozi wa Norwey kitengo cha nishati kushoto kwake ni Paul Kiwele Msimamizi wa mradi wa kuwajengea Uwezo Wataalamu wa Nishati na Tasnia ya Uziduaji(CADESE) wa Wizara ya Nishati na Madini.

Aidha amebainisha kuwa mradi huu utagharimu kiasi cha dola za kimarekani Milioni 15 ambapo Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) watachangia Dola za kimarekani milioni 1 huku wafadhili wengine wakikamilisha kiwango kilichobaki pamoja na kuwaleta wawekezaji mbalimbali kuwekeza katika sekta ya nishati.

Akichangia mada mmoja wa wadau wa nishati nchini Profesa Siza D. Tumbo alisema kuwa Umeme wa jua ni vizuri ukapewa kipaumbele kwani vifaa vyake vinahamishika kwenda sehemu mbalimbali ikiwemo mashambani na hivyo kuchangia katika kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishaji Dkt. Mhandisi Juliana Palangyo (katikati) akiwa katika picha na Katrine Vestbostad kutoka ubalozi wa Norwey kitengo cha nishati kushoto kwake ni Paul Kiwele Msimamizi wa mradi wa kuwajengea Uwezo Wataalamu wa Nishati na Tasnia ya Uziduaji(CADESE) wa Wizara ya Nishati na Madini.

“Kinachohitajika kwa sasa ni kusambaza umeme kwa wananchi, shughuli nyingine zitakazozaliwa kwa uwepo wa nishati hiyo zitajitokeza baada ya umeme kuwekwa” alisisitiza.

Balasankari alizungumzia mkakati wa mpango wa Nishati Endelevu kwa Wote kuwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wan chi zinazohusika na Mpango huo kwa kutoa elimu juu ya kuwavutia wawekezaji katika sekta ya nishati pamoja na kuharakisha utekelezaji wa kupeleka huduma ya nishati kwa wote (SE4all).

Akifunga mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dkt Mhandisi Juliana Pallangyo aliwashukuru wadau kwa kuona umuhimu wa kufanya majadiliano yatakayopelekea utekelezaji wa mikakati endelevu ya kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inapatikana kwa wote.

Imeandaliwa na:

Nuru Mwasampeta,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@mem.go.tz,                                                                               

Tovuti: mem.go.tz