Home » images »

Nishati Jadidifu kuchangia upatikanaji wa umeme wa uhakika

 

Imeelezwa kuwa vyanzo vya nishati jadidifu kama vile upepo, jua, jotoardhi vitachangia upatikanaji wa nishati ya uhakika ya umeme kwa kila  kijiji ifikapo mwaka 2030 kama mpango wa nishati kwa wote unavyofafanua.

Hayo yameelezwa na Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Mhandisi Styden Rwebangila katika mafunzo  kwa  wadau wa nishati jadidifu kuhusu matumizi ya mfumo mpya  wa uhifadhi data  na utoaji taarifa kwa ajili ya  nishati jadidifu ujulikanao kama Tanzania Renewable  Energy  Management Information System (TREMIS) yaliyofanyika jijini Arusha leo.

Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi, Styden Rwebangila (kulia) akibadilishana mawazo na Mtaalam kutoka Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)- Wizara ya Nishati na Madini, Danford Phiri (kushoto) katika mafunzo yaliyokutanisha wadau wa nishati jadidifu jijini Arusha Februari 16, 2017.

Mhandisi Rwebangila alisema kuwa ili nchi ya Tanzania kuingia kwenye orodha ya nchi za kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, nishati ya uhakika ya umeme inahitajika hususan katika kuchochea uwekezaji katika viwanda na kukuza uchumi wa nchi.

Alisema mbali na gesi iliyogunduliwa katika mkoa wa Mtwara na maeneo mengine, nishati ya umeme kutokana na vyanzo vingine kama vile upepo, jua, joto ardhi vinahitajika ili kuongeza kiwango cha umeme katika Gridi ya Taifa.

“ Kuna maeneo ambayo hayajafikiwa na miradi mikubwa ya  Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO) kama visiwani, ambapo Wizara ya Nishati na Madini imeweka utaratibu wa kutumia vyanzo vya nishati mbadala kama jua, upepo na jotoardhi kulingana na maeneo husika ili kila mwananchi afikiwe na huduma ya umme,” alifafanua Mhandisi Rwebangila.

Wadau wa nishati jadidifu wakiendelea na majadiliano katika mafunzo hayo.

Aliendelea kusema kuwa ili kuvutia fursa za uwekezaji, Wizara imeanzisha mfumo mpya wa uhifadhi data  na utoaji taarifa kwa ajili ya  nishati jadidifu ujulikanao kama Tanzania Renewable  Energy  Management Information System (TREMIS) utakaowezesha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kupata taarifa kuhusu fursa za uwekezaji katika nishati jadidifu, sera na taratibu.

Alisema kuwa taarifa za kampuni zote zinazojihusisha na nishati jadidifu, fursa za uwekezaji, sera, sheria na taratibu zitawekwa katika mfumo huo utakaounganishwa na tovuti ya Wizara ili wadau kupata uelewa kabla ya kuwekeza.

Aliendelea kusema kuwa  hatua iliyofikiwa kwa sasa katika maandalizi ya mfumo huo, ni utoaji wa mafunzo na ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa nishati mbadala nchini ambapo mpaka sasa wamekwishafanya zoezi hilo katika Kanda ya Ziwa.

Imeandaliwa na:

Greyson Mwase,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz