Home » images »

Prof. Muhongo azindua Mafunzo ya taa, chaja za mionzi ya jua

 

Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo amezindua Mafunzo ya  namna ya Kutengeneneza Taa na Chaja zinazotumia mwanga wa jua kwa vijana 20  katika Kata ya Nyegina Mkoa wa Mara.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akionesha mfano wa Taa zinazotumia mionzi ya jua ambazo vijana 20 katika Kata ya Nyegina watafundishwa namna ya kuzitengeneza baada ya kuzindua mafunzo hayo. Kulia ni Balozi wa Jmhuri ya Korea nchini, Song Geumyoung na kushoto ni Mkufunzi wa mafunzo hayo Dkt. Hong- Kyu Choi.

Akifungua mafuzo hayo Profesa Muhongo aliwashauri vijana hao kuwa mabalozi wazuri wakati wanapohudhuria mafunzo na kueleza kuwa, yatakuwa chachu katika kupanua wigo wa  wa ajira ikiwemo wahitimu kujiari wenyewe.

Profesa Muhongo aliwataka vijana na wananchi mkoani humo kuweka nguvu kubwa katika elimu kutokana na umuhimu wa elimu  na mchango wake kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumzia kuhusu Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Profesa Muhongo alieleza kuwa, awamu hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia mwezi Machi mwaka huu na kuongeza kuwa, mradi huo utafanywa kwa Awamu na kusisitiza kuwa, adhma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa, ndani ya kipindi cha miaka mitano vijiji vyote nchini viwe vimeunganishwa na nishati hiyo.

” Vijiji vyote vitaunganishwa na nishati ya umeme. Tutasambaza  awamu kwa awamu na lengo letu ni kuhakikisha kuwa, vijiji vyote chini vinaunganishwa na umeme ndani ya kipindi cha miaka mitano. Wale ambao hawajafikiwa awamu ya kwanza na ya pili tutawafikia awamu ya tatu vivyo hivyo mpaka tufikie lengo letu,” amesisitiza Prof. Muhongo.

Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Song Geumyoung ambaye nchi yake imefadhili mafunzo hayo, amesema kuwa,  uwepo wa taa hizo utasaidia upungufu wa umeme hususan maeneo ya vijijini na ambayo bado hayajaunganishwa na nishati hiyo.

Mtaalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya, akizungumza jambo kuhusu utekelezaji wa REA awamu ya Pili na ya Tatu, katika Kata hiyo wakati wa Mkutano wa Waziri wa Nishati na Madini (hayupo pichani) na wananchi wa Kata ya Nyegina.

Aidha, amesema kuwa, mafunzo hayo ni fursa ya ajira kwa wahitimu watakaopata mafunzo hayo ikiwemo nafasi za kuajiriwa na hivyo kuwataka kutilia mkazo mafunzo hayo na kueleza kuwa, mafunzo hayo ni mwanga kwa vijana.

Aidha, ameongeza kuwa,  kutokana na urafiki wa miaka mingi baina ya nchi za Tanzania nasini , hirikinchi hiyo itlea kushirikiana na Tanzania kuhakikisha kwamba taifa linakuwa na umeme wa uhakika.

“Kama ilivyo kwa kaulimbi ya Awamu ya  Tano ya Rais Dkt. John Magufuli, Hapa Kazi Tu’ na mimi napenda kusema tusiende polepole twende ‘Haraka, Haraka”, amesisitiza Balozi  Geumyoung.

Kwa mujibu wa Professa Muhongo mafunzo hayo yanatarajiwa pia kutolewa katika  Kata za Mwirangi, Bukima na Mgango.

Naye Mkufunzi wa Mafunzo hayo Dkt.  Hong- Kyu Choi, amesema kuwa, baada ya kuzifikia Kata zote zilizoainishwa, watachaguliwa wanafunzi bora ambao watakuwa mabalozi wa mafunzo hayo na hivyo kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kufuatilia mafunzo hayo na kuyachukulia kwa uzito mkubwa.

Mbali na kufungua mafunzo hayo, Profesa Muhongo pia amekagua miradi ya umeme Awamu ya Pili inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Kome katika kijiji cha Kome, Kata ya Bwasi.

Mafunzo hayo yamezinduliwa tarehe 20 Februari,2017

Imeandaliwa na:

Asteria Muhozya,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz