Home » images »

Profesa Muhongo aitaka kampuni kuanza uzalishaji madini adimu

 

Serikali imeitaka Kampuni ya PR NG Minerals Limited ya Australia, inayofanya utafiti wa madini adimu (rare earth elements), eneo la Ngualla mkoani Songwe, kukamilisha utafiti huo haraka ili waanze uzalishaji mapema iwezekanavyo.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akizungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya PR NG Minerals Limited, Dave Hammond (kulia), jana, ofisini kwake – Makao Makuu ya Wizara, mjini Dodoma.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alimwambia Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Dave Hammond, aliyemtembelea ofisini kwake mjini Dodoma jana kuwa,  Serikali imedhamiria kuachana na utamaduni au mazoea ya kujikita kwenye uzalishaji wa madini ya kawaida pekee badala yake inataka kuanza uzalishaji wa madini adimu pia ili kuendana na Soko la Dunia.

“Hivi sasa Dunia nzima inageukia kwenye uzalishaji wa madini adimu, hivyo nasi ni lazima tuanze uzalishaji wake mapema iwezekanavyo.”

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akiagana na Mkurugenzi wa Kampuni ya PR NG Minerals Limited, Dave Hammond, baada ya kufanya mazungumzo kuhusu uzalishaji wa madini adimu (rare earth elements). Ujumbe kutoka Kampuni hiyo ulimtembelea Waziri Muhongo ofisini kwake mjini Dodoma jana.

Aidha, Waziri Muhongo aliitaka Kampuni hiyo kuwasilisha Mpango Kazi wake ambao pamoja na mambo mengine utaonesha ni lini uzalishaji utaanza.

Akifafanua umuhimu wa kubainisha Mpango Kazi wa Kampuni hiyo, Profesa Muhongo alibainisha kuwa, baadhi ya wawekezaji katika sekta ya madini hapa nchini, wamekuwa wakishikilia leseni za madini kwa muda mrefu pasipo kuzifanyia kazi hivyo kuilazimu Serikali kuwanyang’anya kwa mujibu wa Sheria ya Madini.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akisisitiza jambo kwa Ujumbe kutoka Kampuni ya PR NG Minerals, waliomtembelea ofisini kwake jana – Makao Makuu ya Wizara, mjini Dodoma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi huyo aliyeambatana na Meneja wa Masoko wa Kampuni husika, Ismail Diwani, alimhakikishia Waziri Muhongo kuwa watakamilisha utafiti wao na kuanza uzalishaji mapema iwezekanavyo.

Mkurugenzi Hammond aliongeza kuwa, kupitia Mradi huo wa madini adimu wa Ngualla, upo uwezekano wa Tanzania kuwa msambazaji mkubwa wa kimataifa wa madini hayo.

Madini adimu yanajumuisha kundi la metali muhimu 17 ambazo ni pamoja na Neodymium, Praseodymium, Scandium na Thulium. Mojawapo ya matumizi yake ni katika magari yanayotumia umeme pamoja na kutengenezea vifaa vya kisasa vya kielektroniki.

Kwa Tanzania, madini adimu yanapatikana katika mikoa ya Songwe, Mbeya na Morogoro.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz