Home » images »

Profesa Muhongo akutana na wenye nia kuwekeza sekta ya nishati nchini

 

Wawekezaji mbalimbali wamemtembelea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ofisini kwake mjini Dodoma na kumweleza nia yao ya kuwekeza kwenye miradi mbalimbali katika sekta ya nishati nchini.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto), akiagana na Ujumbe kutoka Benki ya Stanbic, waliofika ofisini kwake mjini Dodoma, kueleza nia yao ya kuwekeza katika sekta ya nishati nchini. Kushoto kwa Waziri ni Mbunge wa Sumbawanga, Aeshi Hillary.

Akizungumza na Waziri Muhongo, mwakilishi wa Kampuni ya L&T ya India, Sanjay Gupta aliwasilisha nia ya Kampuni hiyo ya kujenga njia ya kusafirisha umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Stanbic, Thomas Buonga akiwa ameambatana na Mkuu wa Sekta inayoshughulikia masuala ya Umma wa Benki hiyo, Noella Kimaro, walimweleza Waziri kuwa wanaangalia fursa ya kuwekeza katika miradi ya sekta ya nishati.

Naye, mwekezaji kutoka Denmark, Malte Meyer, akiwa amefuatana na Ofisa kutoka ubalozi wa nchi hiyo, Derrick Katunzi, alisema nia ya kampuni yake ni kuwekeza katika sekta ya nishati hususan uzalishaji wa umeme kwa kutumia upepo.

Waziri Muhongo aliwakaribisha wawekezaji hao na kuwahakikishia kupata ushirikiano kutoka serikalini endapo watakidhi vigezo stahiki vya uwekezaji vilivyowekwa.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@mem.go.tz,                                             

Tovuti: mem.go.tz