Profesa Muhongo, Dkt. Kalemani watoa maagizo kwa Wizara / Taasisi

 

Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo ametaka Watumishi wa Wizara na Taasisi kuelewa na kujadili namna Sekta za Nishati na Madini zitakavyosaidia kufikia lengo la Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025, kutokana na umuhimu wa Sekta hizo katika kufikia Dira hiyo.

Alisema kuwa majadiliano hayo katika sekta za Nishati na Madini yatapelekea kufikia lengo la Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 na kuifanya Tanzania kuwa na umeme wa kutosha na nchi yA Kipato cha Kati.

Profesa Muhongo aliyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Nishati na Madini lililofanyika kwa Video Conferencing kutoka vituo vya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza na kushirikisha Wawakilishi kutoka Wizara, Taasisi na Ofisi za Madini za Kanda.

Aliwataka Watumishi hao kujadili namna Sekta hizo zitakavyowezesha ongezeko la ukusanyaji wa maduhuli mbalimbali yatakayosaidia kuchangia katika Bajeti Kuu ya Serikali.

Akizungumzia Sekta ya Madini, alitaka sekta hiyo ijikite zaidi katika mikakati ambayo itawezesha Taifa kunufaika kutokana na mchango wa madini Mapya kama Graphite ambayo matumizi   yake ni makubwa na yanahitajika viwandani na katika teknolojia mbalimbali duniani na kuongeza kuwa, madini hayo yatawezesha kuvutia uwekezaji mpya.

Aidha, alieleza kuhusu mchango wa asilimia nne (4) wa Sekta ya Madini katika Pato la Taifa na kueleza kuwa, mchango wa sekta hiyo bado ni kidogo na hivyo kuwataka Watalaam husika kuweka mikakati na malengo zaidi itakayowezesha mchango zaidi wa sekta hiyo.

“Tarehe 1 Julai mwaka huu tutafanya kikao kujadili madini mapya ya viwandani  yanayohitajika Duniani  ambayo tunayo hapa nchini.  Tujadili na tuweke mikakati ya namna ya kutoka hapa tulipo kupitia madini hayo,” alisisitiza Profesa Muhongo.

Akizungumzia Sekta ya Nishati aliwataka Wataalam kujadili na kujipanga kuhusu namna Taifa litakavyo tumia vyanzo vipya vya kuzalisha umeme ambavyo vinapatikana nchini ikiwemo Mkaa ya Mawe na Nishati Jadidifu.

“Lazima tujenge picha kubwa ya namna gani tupate umeme mwingi kutoka vyanzo tulivyonavyo. Namna ya kusafirisha umeme mwingi na kusambaza umeme mkubwa. Pamoja na mambo mengi mtakayojadili, masuala muhimu ya sekta hizi lazima yajadiliwe,” alisema Prof. Muhongo.

Pia alitaka Wataalam husika kuwaandaa Watanzania kuhusu namna ya kushiriki katika miradi mipya ikiwemo Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG), Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga na Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Safi kutoka Dar es Salaam Tanzania hadi Ndola nchini Zambia.

Aidha, Profesa Muhongo alisistiza uadilifu kwa Watumishi wa Wizara na Taasisi, wakati wa kutekeleza majukumu yao ikiwemo pia kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa weledi na kusisitiza kuhusu kuzingatiwa kwa kustahiki za watumishi.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE Wizara ya Nishati na Madini ambaye anamaliza muda wake, Marcelina Mshumbusi akisoma risala ya watumishi katika mkutano huo, alieleza umuhimu wa chombo hicho kwa watumishi na kuipongeza Wizara kwa kuzingatia maslahi ya wafanyakazi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani wakati akifunga mkutano huo, alipongeza namna Baraza hilo lilivyoendeshwa kwani limesaidia kupunguza gharama.

Dkt. Kalemani aliwataka Watumishi na Watendaji kujiandaa kwa utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2017/18 na kuongeza kuwa, kila mtumishi ana umuhimu wake katika utekelezaji wa Bajeti hiyo.

Akieleza utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka 2016/17, alisema kuwa, yapo maeneo ambayo wizara imefanya vizuri sana kuwataka watumishi kujipanga kwa utekelezaji wa maeneo ambayo hayakutekelezwa kikamilifu.

Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Nishati na Madini lilifanyika tarehe 12 Aprili, 2017.

Imeandaliwa na:

Asteria Muhozya na Rhoda James,

Maafisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@mem.go.tz,                                                                               

Tovuti: mem.go.tz