Home » images »

Serikali kukusanya mrabaha wa shilingi milioni 466.4 kutoka mnada wa pili wa Tanzanite

 

Imeelezwa Serikali itakusanya mrabaha wa Dola za Marekani 210,114.36 sawa na Shilingi 466,453,871.43  kutokana na mauzo ya madini ya Tanzanite yaliyofanyika katika Mnada wa Pili wa Kimataifa wa madini hayo jijini Arusha.

Viongozi mbalimbali wakifuatilia hafla ya kutangaza washindi wa Mnada wa Pili wa Kimataifa wa madini ya Tanzanite uliofanyika jijini Arusha. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe na Mkuu wa wilaya Simanjiro, Zephania Chaula.

Hayo yalielezwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthamini wa Madini ya Almasi na Vito kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo, katika hafla ya kutangaza washindi wa mnada huo wa Tanzanite uliofanyika katika kituo cha Jemolojia tarehe 12 Februari, 2017.

Kalugendo alisema kuwa mrabaha huo unatokana na jumla ya gramu 990,039.04 za Tanzanite ghafi kuuzwa kwa  Dola za Marekani 4,202,287.13 katika mnada huo. Aliongeza kuwa hiyo ni sawa na asilimia 99.9 ya madini yote yaliyopelekwa  kwa ajili ya mauzo.

Viongozi mbalimbali walioshiriki hafla ya kutangaza washindi wa Mnada wa Pili wa Kimataifa wa madini ya Tanzanite uliofanyika jijini Arusha. Wa kwanza kushoto Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera, wa pili ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe, wa Tatu kushoto ni Mkuu wa wilaya Simanjiro, Zephania Chaula na wa kwanza kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Mhandisi Hamis Komba.

Aliongeza kuwa kampuni tatu zinazochimba madini ya Tanzanite zilizopeleka madini hayo kwa ajili ya mauzo ni  Tanzanite One Mining Company Ltd, Mathias J Lyatuu Mining na Tanzanite Africa Ltd ambapo zilipeleka jumla ya gramu 990,444.04 za madini ghafi kwenye mnada huo.

Aidha Kalugendo aliongeza kuwa kutokana na mauzo hayo ya Tanzanite Halmashauri ya Wilaya ya Simajiro ambako madini hayo yanachimbwa, inatarajia kulipwa shilingi 27,987,232.29 kama kodi ya huduma.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera, ambaye alikuwa ni mgeni rasmi katika hafla ya kutangaza washindi wa Mnada wa Pili wa Kimataifa wa madini ya Tanzanite uliofanyika jijini Arusha, akihutubia wageni mbalimbali walioshiriki kwenye mnada huo. Kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Prof. James Mdoe na wa kwanza kushoto ni Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje.

Kalugendo alisema kuwa mnada huo ulihudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ambapo Kampuni 68 kutoka nchi saba duniani ambazo ni Tanzania, Kenya, India, Sri Lanka, China, Uswisi na Ujerumani zilishiriki..

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dkt. Joel Bendera, ambaye alikuwa ni mgeni rasmi katika hafla hiyo, alitoa wito kwa Wizara ya Nishati na Madini kuwa na mpango wa kuongeza thamani madini ya vito hapa nchini badala ya kusafirisha nje ya nchi yakiwa ghafi kwani inapunguza ajira kwa vijana wa kitanzania.

Wadau mbalimbali walioshiriki hafla ya kutangaza washindi wa Mnada wa Pili wa Kimataifa wa madini ya Tanzanite uliofanyika jijini Arusha. Wa kwanza na wa pili kushoto ni wamiliki wa mgodi wa Tanzanite One, Faisal Shahbhai na Hussein Gonga. Wa tatu kutoka kulia ni Mhasibu Mkuu kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Beatrice Lupi. Mgodi wa Tanzanite One unamilikiwa na kampuni ya Sky Associates kwa ushirikiano na STAMICO, kila moja akiwa na hisa asilimia 50.

“Fanyeni jitihada hata za kuwashawishi hawa wanunuzi wa nje wakishirikiana na wanunuzi wa ndani kuwekeza hapa nchini katika viwanda vya kukata madini ya vito ili kuwaongezea ajira vijana wetu”, alisema  Dkt.Bendera.

Dkt. Bendera pia, aliishauri Wizara ya Nishati na Madini kuharakisha mchakato wa ujenzi wa jengo la madini latika eneo la EPZ wilayani Mererani ili kufanikisha zoezi zima la kuchakata madini karibu na eneo ambako madini hayo yanachimbwa

Kuhusu suala la uhaba wa baruti zinazotumika kuvunjia miamba migodini, Mkuu wa mkoa wa Manyara aliitaka Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha kwamba kunakuwa na ushindani  wa wauzaji wa baruti ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa bidhaa hizo kutokana na kuwa na wauzaji wachache wa baruti.

Aidha aliipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kutambua umuhimu wa kuendeleza mnada huo wa madini ya Tanzanite  kwa mara ya pili  ambapo hamasa ya ushiriki  wa mnada huo imeongezeka zaidi na idadi ya wafanyabiashara imeongezeka.

Imeandaliwa na:

Teresia Mhagama na Zuena Msuya,

Maafisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz