Home » images »

Serikali kutumia zaidi ya bilioni 35 kusambaza umeme Shinyanga

 
  • Ni kupitia Mradi wa REA III

Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 35.25 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika Mkoa wa Shinyanga.

Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi huo, uliofanyika katika Kijiji cha Negezi wilayani Kishapu, hivi karibuni.

Mhandisi Nyamo-Hanga alisema kuwa, fedha hizo zitatumika kusambaza umeme katika vijiji 351 vya Mkoa huo ambavyo bado havijapata huduma hiyo na hivyo kufanya vijiji vyote 509 vya Mkoa wa Shinyanga kuwa na umeme.

Mkandarasi Mrisho Masoud kutoka Kampuni ya M/s OK Electronics and Electric Limited (katikati) na timu ya wafanyakazi wa Kampuni hiyo, wakitambulishwa kwa viongozi pamoja na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kuwa ndiyo watakaotekeleza Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) Mkoa wa Shinyanga. Pamoja nao ni Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, Mhandisi Bengiel Msofe (kushoto) na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Sotco Nombo (wa pili kutoka kushoto)

Akifafanua, alisema kwamba, utekelezaji wa Mradi wa REA III umegawanyika katika awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza, inayotarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa; itahusisha kusambaza umeme katika vijiji 149. Aliongeza kuwa, vijiji 202 vitakavyobaki, vitapatiwa umeme katika awamu ya pili ya Mradi wa REA III itakayokamilika mwaka 2021.

Mkurugenzi Nyamo-Hanga, alimtaja Mkandarasi atakayehusika na utekelezaji wa Mradi huo katika Mkoa wa Shinyanga kuwa ni M/s OK Electronics and Electric Limited na kusema kuwa ataanza kazi mara moja.

Aliwashauri wananchi watakaounganishiwa umeme katika Awamu hii ya Tatu, kukamilisha mapema utandazaji wa nyaya katika nyumba zao ili Mkandarasi atakapofika katika maeneo yao wawe tayari kulipia na kupatiwa huduma hiyo muhimu.

Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga, akizungumza na wananchi wa Kishapu mkoani Shinyanga (hawapo pichani), wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) Mkoa wa Shinyanga.

Aidha, Mhandisi Nyamo-Hanga aliwahimiza wananchi kutoa maeneo kwa ajili ya kupitishia miundombinu ya kusambaza umeme bila kudai fidia kama mchango wao kwenye mradi huo wa maendeleo.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (katikati), akibonyeza kitufe maalum kuashiria uzinduzi rasmi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) Mkoa wa Shinyanga. Wanaoshuhudia ni Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Shinyanga ambaye pia ni Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige na Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi.

Alizikumbusha Serikali za Kata na Vijiji kubainisha maeneo maalum ya viwanda ambayo katika mradi husika, yatafikishiwa miundombinu ya umeme mkubwa unaolenga kuwezesha wajasiriamali vijijini kupatiwa umeme utakaowezesha kuanzishwa kwa viwanda vidogo vidogo na vikubwa kwa gharama nafuu.

Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, unalenga kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji 7,873 katika Wilaya na Mikoa yote ya Tanzania Bara ambavyo bado havijafikiwa na umeme.

Kwa mujibu wa taarifa ya maeneo rasmi ya kiserikali kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Tanzania Bara ina Vijiji 12,268 ambapo kati yake, vilivyofikiwa na umeme hadi Juni 2016 ni 4,395 sawa na asilimia 36.

Kati ya Vijiji 7,873 ambavyo havijapata umeme, Vijiji 7,697 vimepangwa kupatiwa umeme wa gridi na Vijiji 176 pamoja na Viziwa, vitapatiwa umeme wan je ya gridi kwa kuwa ndiyo njia muafaka ya kuvipatia umeme kwa sasa.

Mradi huu umepangwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2016/17 hadi 2020/21.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

BaruaPepe: info@mem.go.tz                                             

Tovuti: mem.go.tz