Home » images »

Serikali yautaka mgodi wa urani kuanza uzalishaji

 
  • Yasisitiza kutosafirisha mchanga nje ya nchi

Serikali imeuagiza Mgodi wa Mantra uliopo Namtumbo mkoani Ruvuma, kuanza uzalishaji wa madini ya urani ndani ya miaka miwili kuanzia sasa ili wananchi waweze kunufaika kama ilivyokusudiwa.

Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani, alipotembelea Mgodi huo akiwa katika ziara ya kazi mkoani humo, kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Wizara yake.

Dkt Kalemani alisema kuwa, kulingana na mpango-kazi uliokuwepo, Mgodi huo ilikuwa ufunguliwe ndani ya miezi 24 tangu ulipopatiwa leseni ya uchimbaji, Aprili 5, mwaka 2013 lakini uzalishaji haujaanza hadi sasa.

Mmoja wa Wataalam wa Kampuni ya Mantra inayomiliki Mgodi wa madini ya Urani uliopo Namtumbo mkoani Ruvuma, Leonid Serov (kushoto), akimweleza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto) namna utaratibu/njia ya uvunaji madini ya urani ijulikanayo kitaalam kama In-Situ Recovery (ISR) inavyofanya kazi. Kampuni ya Mantra inafanya utafiti wa majaribio ya kutumia njia hiyo ili waweze kuitumia watakapoanza uzalishaji. Naibu Waziri amesisitiza kutumia njia hiyo kwani ni rafiki wa mazingira.

Mmoja wa Wataalam wa Kampuni ya Mantra inayomiliki Mgodi wa madini ya Urani uliopo Namtumbo mkoani Ruvuma, Leonid Serov (kushoto), akimweleza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (wa pili kutoka kushoto) namna utaratibu/njia ya uvunaji madini ya urani ijulikanayo kitaalam kama In-Situ Recovery (ISR) inavyofanya kazi. Kampuni ya Mantra inafanya utafiti wa majaribio ya kutumia njia hiyo ili waweze kuitumia watakapoanza uzalishaji. Naibu Waziri amesisitiza kutumia njia hiyo kwani ni rafiki wa mazingira.

“Mlipewa miaka miwili ya ujenzi ambayo imeshapita. Huu ni mwaka wa Nne sasa, hivyo tunasema anzeni uzalishaji ndani ya miaka miwili ijayo.”

Akifafanua kuhusu kutoa miaka miwili ili Kampuni hiyo iwe imeanza uzalishaji, Naibu Waziri alieleza kuwa, mpango wa kisheria na ule wa ujenzi, miaka miwili imeshapita hivyo ni haki kwa Serikali kuitaka Kampuni hiyo kuanza kuzalisha ili ianze kulipa Kodi kwa Serikali na kuajiri watanzania.

Ilielezwa kuwa, Mgodi wa Mantra unaweza kuajiri zaidi ya watu 1500 katika hatua za mwanzo za ujenzi na zaidi ya watu 2000 ukianza uzalishaji baada ya ujenzi, jambo ambalo Naibu Waziri anasema kuwa ni la manufaa kwa watanzania.

Aidha, Naibu Waziri alitaja faida nyingine kubwa ya Mradi huo wa Urani itakayopatikana baada ya kuanza uzalishaji kuwa ni mapato kwa Serikali yatakayotokana na ushuru, kodi na tozo mbalimbali ambazo kisheria haziwezi kutozwa ikiwa Mradi haujaanza kuzalisha.

“Dhamira yetu ni kupata kodi ili tuijenge nchi yetu kwani bila kodi hakuna Serikali inayoweza kukua kiuchumi. Hivyo tunawahimiza Mantra mfungue Mgodi ili muanze kulipa kodi na kuajiri wafanyakazi wengi zaidi ili watanzania wanufaike,” alisisitiza.

Akizungumzia sababu zinazotajwa na wamiliki wa Mgodi kuwa zinachangia kuchelewesha kuanza uzalishaji, Naibu Waziri alieleza kuwa sababu ya kwanza inayolalamikiwa ni kushuka kwa bei ya madini hayo katika Soko la Dunia, ambapo alifafanua kuwa sababu hiyo yaweza kuwa kweli lakini haina uzito wa kufanya maamuzi ya kuacha kuwekeza.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kushoto), akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Mgodi wa Mantra alipotembelea Mgodi huo hivi karibuni akiwa katika ziara ya kazi mkoani Ruvuma kukagua miradi inayosimamiwa na Wizara yake.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt Medard Kalemani (kushoto), akisisitiza jambo kwa Viongozi wa Mgodi wa Mantra alipotembelea Mgodi huo hivi karibuni akiwa katika ziara ya kazi mkoani Ruvuma kukagua miradi inayosimamiwa na Wizara yake.

Naibu Waziri alifafanua kuwa, suala la kupanda na kushuka kwa bei ni jambo la kawaida, hivyo aliutaka uongozi wa Mgodi wa Mantra kuhakikisha Mgodi unafunguliwa mapema.

“Suala la kushuka kwa bei ni la kiulimwengu zaidi hivyo ni lazima twende mbele. Mnapochelewesha kuanza uzalishaji, mnatupa Serikali shida,” alisisitiza.

Sambamba na agizo la kuanza uzalishaji, pia Naibu Waziri aliitaka Kampuni ya Mantra kuzingatia taratibu, sheria na kanuni ambazo Serikali imeziweka kwa wawekezaji nchini ikiwemo ya kutosafirisha mchanga kwenda nje ya nchi na badala yake wajenge Kiwanda husika nchini.

“Serikali inatambua kuwa, kwa Mradi huu wa Urani, mnahitaji kufanya usafishaji na kuchuja madini hayo. Hata hivyo, hatutarajii usafishaji wa mchanga wa aina yoyote ufanyike nje ya nchi kwa kipindi cha kuanzia miaka minne hadi mitano ijayo, hivyo ninyi muanze maandalizi mapema.”

Awali, akitoa taarifa ya Kanda ya Ziwa Nyasa kwa Naibu Waziri, Kaimu Kamishna wa Madini anayesimamia Kanda hiyo, Fredy Mahobe alisema kuwa, Mradi wa Mantra ni moja ya miradi ambayo inategemewa kuleta manufaa makubwa kwa Taifa kupitia kodi, ajira na mapato mbalimbali, pindi utakapoanza uzalishaji.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz