Home » images »

Serikali yazuia uchimbaji kwenye Mto Muhuwesi

 

Serikali imezuia shughuli za uchimbaji wa madini ya vito kwenye Mto Muhuwesi wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma hadi hapo taarifa za kitaalamu zitakapotolewa mara baada ya kukamilika kwa zoezi la tathmini na ukaguzi.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akitoa maelekezo kwa Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Nyasa, Mhandisi Fred Mahobe wakati wa ziara yake kwenye maeneo unakotiririsha maji mto Muhuwesi.

Agizo hilo limetolewa jana wilayani humo na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipofanya ziara kwenye mto huo ili kujionea hali ya eneo husika kufuatia ajali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Kanje Ally na majeruhi mmoja ambao waliingia na kuanza kuchimba ndani ya mto.

Kwa mujibu wa taarifa ya Afisa Madini Mkazi wa Wilaya ya Tunduru, Mhandisi Fredrick Mwanjisi, zaidi ya watu sita walivamia eneo hilo la mto kufanya shughuli za uchimbaji wa madini kinyume cha taratibu kutokana na kutokuwa na vibali vilivyowaruhusu kufanya shughuli ya uchimbaji katika eneo hilo.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya vito wilayani Tunduru wakati alipotembelea eneo la Mto Muhuwesi.

Taarifa hiyo ilieleza kwamba shughuli za uchimbaji wa madini ndani ya Mto Muhuwesi zilisimamishwa tangu mwaka 2014 kufuatia pingamizi kutoka kwa Mamlaka ya Bonde la mto Ruvuma na Bonde la Kusini kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa rasilimali za Maji Namba 11 ya mwaka 2009 na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira namba 20 ya mwaka 2004.

Kufuatia taarifa hiyo na baada ya kujionea hali halisi na kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo pamoja na viongozi wao, Waziri Muhongo aliagiza kusitisha haraka shughuli zote za uchimbaji madini kwenye mto huo hadi hapo taarifa ya tathmini ya athari ya shughuli ya uchimbaji kwa mazingira ya Mto Muhuwesi itakapokamilishwa na kuwasilishwa na wataalam kutoka Mamlaka ya Bonde la Mto Ruvuma, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Wizara ya Nishati na Madini (MEM).

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akimsikiliza Afisa Madini Mkazi, Tunduru, Mhandisi Fredrick Mwanjisi akielezea kuhusiana na shughuli za uchimbaji wa madini ya vito zilizokuwa zikifanyika kwenye Mto Muhuwesi, wilayani Tunduru.

Ili kuhakikisha suala hilo linapata ufumbuzi wa haraka, Waziri Muhongo alitoa miezi mitatu kwa wataalam kutoka Mamlaka hizo wawe wamewasilisha taarifa hiyo kwake na kwa uongozi wa Wilaya ya Tunduru. “Tarehe 30 Mei, 2017 wataalamu watakaohusika na ukaguzi wanatakiwa kuwasilisha taarifa yao kwa Mkuu wa Wilaya bila kukosa; hatuwezi kuendelea kukaa kimya,” alisema Waziri Muhongo.

Akisisitiza kuhusu agizo hilo la kusimamisha uchimbaji ndani ya mto, Waziri Muhongo alibainisha kwamba kwa uzoefu alionao hajawahi kuona taifa lolote duniani likifanya shughuli za uchimbaji wa madini kwenye mito lakini alisema anatoa muda kwa wataalam husika kufanya majadiliano na kukagua athari za shughuli za uchimbaji wa madini kwenye mto huo.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini ya vito wilayani Tunduru wakati alipotembelea eneo la Mto Muhuwesi.

Waziri Muhongo vilevile aliziagiza Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Nyasa, Songea na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi, Tunduru kuandaa orodha ya leseni zote kwenye Wilaya inayobainisha leseni zinazofanyiwa na zisizofanyiwa kazi na kuikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Tunduru ili kuruhusu wenye kuhitaji waweze kuyaombea leseni.

“Kuna wachimbaji walipewa maeneo lakini hawayaendelezi, wanastahili kunyang’anywa ili yakabidhiwe kwa vikundi vilivyo tayari kufanya uchimbaji,” alisema Profesa Muhongo.

Aliwataka wachimbaji watakaopewa maeneo wahakikishe wanafuata sheria za uchimbaji na ushauri wa kitaalam unaotolewa na wataalam kutoka Ofisi za madini ili kuepusha ajali  zinazoepukika.

Waziri Muhongo, alishauri wabunge na madiwani wa maeneo husika yenye shughuli za uchimbaji madini kufanya kikao kitakachowajumuisha wataalamu kutoka Ofisi za Madini Tunduru na Kanda ya Ziwa Nyasa na ofisi ya Mkuu wa Wilaya na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili kujadili suala la ushuru wa huduma (service levy) wanazopaswa kulipwa kutokana na uchimbaji na uuzaji wa madini Wilayani Tunduru.

Imeandaliwa na:

Mohamed Saif,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz