Home » images »

STAMICO yaanza kuuza makaa ya mawe

 

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza rasmi kuuza makaa ya mawe yanayozalishwa katika Mgodi wake wa Kabulo ili kukidhi mahitaji ya watumiaji wakiwemo viwanda vya saruji na nguo na hivyo kukuza Pato la Taifa. STAMICO ilianza uzalishaji wa majaribio wa makaa ya mawe katika mgodi wa Kabulo uliopo Kijiji cha Kapeta, Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe mnamo tarehe 30 Aprili 2017 na mpaka sasa imeweza kuzalisha tani 6,197.

Makaa ya mawe Kabulo.

Akihojiwa na Mwandishi wa Habari hii, mara baada ya zoezi la uuzaji makaa ya mawe kuanza rasmi huko Kabulo (6 Julai 2017), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Mhandisi Hamis Komba, alisema kuwa Shirika kupitia mradi wake wa makaa ya mawe wa Kabulo, sasa linaweza kukidhi mahitaji ya watumiaji wote wa makaa ya mawe nchini katika kipindi cha miaka 100 mfululizo kutokana na kuwepo kwa mashapo ya kutosha (mineral resources) na nyenye ubora wa juu.

Komba alisema kuwa, matarajio ya Shirika ni kuongeza kiwango cha uchimbaji wa makaa ya mawe kutoka tani 600 hadi tani 1000 kwa siku, hatua ambayo itaiwezesha STAMICO kuzalisha zaidi ya tani 300,000 kwa mwaka. “Nchi yetu ina rasilimali nyingi za madini yakiwemo makaa ya mawe, hivyo tunapenda kuwahakikishia wenye viwanda vinavyotumia makaa hayo hususan viwanda vya Saruji (Cement), kwamba nchi ina makaa ya kutosha hivyo Serikali haitoshindwa kutosheleza mahitaji na makaa ya mawe huku ikitekeleza kwa vitendo azma yake kujenga Tanzania yenye viwanda, ili kukuza uchumi wa Taifa,” alifafanua Mhandisi Komba.

Aidha, Aliwataka wenye viwanda nchini, kuwasilisha maombi ya kununua malighafi ya makaa ya mawe, ili STAMICO iweze kuwauzia makaa hayo, ambayo yana viwango vya ubora vinavyofaa katika uzalishaji wa nishati ya umeme viwandani. Aliongeza kuwa, hivi sasa Shirika linaendelea kuimarisha mradi huo wa Kabulo, kwa kuboresha miundombinu, maabara ya kudhibiti ubora wa makaa na kununua mashine mpya (Crusher) kwa ajili ya kuponda makaa, kulingana na mahitaji mahsusi ya vipimo vinavyhitajiwa na wateja katika soko.

Makaa ya mawe Kabulo

“Kwa sasa tunajitahidi kutatua changamoto zilizopo katika utekelezaji wa mradi huu ikiwa ni pamoja na mtaji mdogo, mabadiliko ya hali ya hewa hasa nyakati za mvua na ubovu wa kipande cha barabara yenye urefu wa zaidi ya kilomita 15 kutoka katika eneo la mgodi, mpaka eneo la mauzo, ambapo barabara hiyo haiwezi kumudu malori ya zaidi ya uzito wa tani 15 kupita,” alibainisha Mhandisi Komba.

Awali Mratibu wa Mradi wa Makaa ya Mawe wa KabuloKiwira, Alex Rutagwelela, alisema amefurahishwa na matokeo chanya ya mradi huo ya kufikia hatua ya uuzaji makaa ya mawe, kwani ni fursa nzuri kwa Shirika, baada ya Serikali kuweka zuio la kuagiza makaa ya mawe kutoka nchi za nje; wakati nchi ikiwa na makaa mengi ya mawe ardhini. Alisema STAMICO kupitia mradi huo, itaendelea kuimarisha viwango vya uzalishaji wa makaa ya mawe ili kuwafikia wateja wote kulingana na mahitaji yao “Uwezo wetu na utaalam katika uchimbaji makaa ya mawe ni wa kimkakati ili kuweza kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.

Lengo kuu la mradi huu ni kutosheleza mahitaji ya kuzalisha umeme wa viwango mbalimbali katika Mradi wa Umeme wa Kiwira na pia kutosheleza mahitaji ya Viwanda nchini vikiwemo vya saruji.” Naye Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa STAMICO, Deusdedith Magala aliwasihi watumishi na wataalam wa Shirika hilo, kuendelea kujifunga mkanda na kufanya kazi kwa bidii ili kuivusha salama STAMICO katika kipindi hiki cha mpito, ambapo Shirika linafufua miradi yake ya uchimbaji madini; itakayoleta mafanikio makubwa na yenye maslahi mapana kwa Taifa.

Makaa ya mawe Kabulo.

Magala alisema kuwa, STAMICO imeweza kuanza uzalishaji wa makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo kwa kutumia mtaji mdogo na kubana matumizi; hatua ambayo imedhihirisha kwamba STAMICO imethubutu na inaweza kutekeleza miradi kwa wakati. Awamu ya kwanza ya Mradi wa uchimbaji makaa ya mawe wa Kabulo inatekelezwa kupitia leseni zake mbili za uchimbaji mdogo wa madini Primary Mining Licences (PMLs) zilizopo ndani ya leseni ya utafiti ya Kabulo zenye ukubwa wa Hekta 16.52.

Leseni hizo mbili za Uchimbaji wa Awali wa Madini katika eneo hilo la Kabulo, zina zaidi ya tani milioni 35 zilizothibitishwa za mashapo ya makaa ya mawe, yaliyoko karibu na uso wa ardhi, katika mgodi huo wa Kabulo.

Imeandaliwa na:

Koleta Njelekela-STAMICO,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@mem.go.tz,                                                                               

Tovuti: mem.go.tz