STAMICO yaanza maandalizi ya uchimbaji wa makaa ya mawe Kabulo

 

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeanza maandalizi ya mradi wa uchimbaji makaa ya mawe katika eneo la Kabulo Wilayani Ileje Mkoa wa Songwe, ili kuanza kutekeleza mradi huo ifikapo mwishoni mwa mwezi Aprili, 2017.

Awamu ya kwanza ya Mradi huo itatekelezwa kupitia leseni zake mbili za uchimbaji mdogo wa madini Primary Mining Licences (PMLs) zilizopo ndani ya leseni ya utafiti ya Kabulo zenye ukubwa wa Hecta 16.52.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Uchorongaji wa STAMICO, Alex Rutagwelela ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu maendeleo ya maandalizi ya eneo la Mradi, baada ya kurejea kutoka Kiwira, alikokwenda kuratibu kazi ya kutathimini kiwango cha mashapo yaliyopo katika leseni hizo za uchimbaji mdogo-Kabulo.

Rutagwelela alisema kuwa leseni hizo mbili za Uchimbaji wa Awali wa Madini katika eneo hilo la Kabulo zina tani  zipatazo 241,865 za mashapo ya makaa ya mawe yaliyoko karibu na uso wa ardhi ambayo yataruhusu Uchimbaji wa Mgodi wa Wazi (Open pit mining) kufanyika.

Aidha Rutagwelela alibainisha kuwa STAMICO ina mpango wa  kufanya kazi za uchorongaji miamba katika mlima wa Kabulo ili  kuongeza kiwango cha mashapo  ya  Makaa ya Mawe kilichopo chini ya ardhi katika mlima wa Kabulo ambacho kwa sasa kinadiriwa kufika tani milioni 85.

“Uchimbaji huu, ambao utaanzia kwenye mlima wa Kabulo na baadae mlima wa Ivogo, utaiwezesha STAMICO kuzalisha makaa ya mawe na hivyo kupunguza uhaba wa madini hayo nchini ambayo ni moja ya vyanzo vya nishati ya umeme. Makaa ya mawe hutumika kama moja ya vyanzo vya Nishati katika shughuli za uzalishaji viwandani vikiwemo viwanda vya Saruji nchini” alifafanua Mkurugenzi Rutagwelela.

>>Soma Zaidi>>