STAMICO yajipanga kufufua mgodi wa makaa ya mawe Kiwira

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Balozi Alexander Muganda alisema Bodi ya Shirika hilo imejipanga kufufua uzalishaji wa makaa ya mawe katika Mgodi wa Kiwira haraka iwezekanavyo ili kuuwezesha mgodi huo kuingiza mapato kwa Shirika na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.

Balozi Muganda aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihitimisha ziara ya wajumbe wa bodi mpya ya STAMICO katika Mgodi wa Makaa ya Mawe-Kiwira iliyotembelea mgodi huo ili kukagua mazingira na kujionea changamoto zilizopo katika kuelekea kuufufua mgodi huo.

Balozi Muganda amesema Bodi ya STAMICO iliyoanza kazi rasmi Julai 2016, imetembelea miradi yote inayoendeshwa moja kwa moja na Shirika au kupitia kampuni tanzu za shirika hilo ili kuona namna ya kuiendesha miradi hiyo kwa manufaa na hivyo kuiwezesha STAMICO kujiendesha kwa faida.

Amesema kwa kuwa gharama za kufufua Mgodi wa Kiwira ni kubwa sawa na Dola za Kimarekani milioni 7.56, dhamira ya sasa ya Bodi ni kuanza uzalishaji wa makaa ya mawe na kuuza wakati Shirika likiendelea na mipango mingine ikiwemo kufufua mitambo ya uzalishaji umeme wa megawati 6 utakaounganishwa katika gridi ya Taifa na kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Songwe na Mbeya.

“Mpango mkubwa wa baadaye wa STAMICO juu ya Kiwira ni kukuza uzalishaji wa makaa ya mawe kutoka tani 150,000 za makaa ghafi kwa mwaka hadi kufikia tani 1,500,000 kwa mwaka hatua ambayo pia italiwezesha Shirika kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawati sita hadi kufikia megawati 200” Alifafanua Balozi Muganda.

Awali Kaimu Meneja Mkuu wa mgodi Mhandisi Aswile Mpamba aliieleza Bodi mpya ya STAMICO kuwa mgodi huo ulisimamisha uzalishaji wa makaa ya mawe mwaka 2008 na uzalishaji wa umeme mwaka 2009, jambo lililopelekea Serikali kuufunga kabisa mgodi huo mwaka 2012.

Hatua hiyo iliisababisha Serikali kuajiri wafanyakazi 44 kwa ajili ya kufanya uangalizi wa mgodi, kulinda mali ya umma (Care and Maintanance) na kuboresha mazingira ya mgodi wakati Serikali ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa kuufufua mgodi huo. Mgodi una wafanyakazi 39 tu kwa sasa baada ya wafanyakazi watatu kustaafu na wengine wawili kufariki dunia.

Mapamba amebainisha kuwa katika vipindi viwili tofauti kati ya mwaka 2014 na 2016 STAMICO imeunda timu ya wataalam waliofanya tathimini ya kina juu ya ufufuaji uzalishaji makaa ya mawe Kiwira katika mashapo ya Ivogo na Kabulo pamoja na kuanza kwa uzalishaji umeme.

Pamoja na mambo mengine, timu hiyo ya wataalam ilitathimini kuhusu hali halisi ya uchakavu wa mitambo, mgodini, kituo cha umemekinu cha kusafishia makaa ya mawe, magari na makazi.

“Timu hiyo imebaini kuwa Mgodi wa Kiwira unaweza kuanza uzalishaji wa awali wa tani 150,000  za makaa ghafi kwa mwaka na megawati sita za umeme kutoka katika kituo chake cha uzalishaji umeme kilichomo ndani ya eneo la mgodi” Alifafanua Mhandisi Mapamba.

Aidha Mhandisi Mapamba ameiomba Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO kusaidia kuhakikisha kuwa mtaji wa ufuaji shughuli za uzalishaji makaa ya  mawe na umeme unapatikana kwa wakati muafaka ili kuokoa kuendelea kuchakaa kwa mitambo ambayo hauijafanya kazi kwa muda mrefu.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO Mhandisi Hamis Komba amesema baada ya kutembelea mgodi wa Kiwira ameweza kuujua vizuri na kupata mwelekeo wa kitaaluma wa kinachotakiwa kufanyika katika kuifufua Kiwira tofauti na taarifa za awali alizozisoma kwenye makabrasha baada ya kuteuliwa rasmi kushika wadhifa huo Januari 3, 2017.

“Bodi ya STAMICO imejionea jinsi mgodi ulivyo na kwamba makaa ya mawe yanavyoweza kupatikana kwa urahisi kufuatia hazina iliyopo katika mgodi huo ambapo Kabulo peke yake inakadiriwa kuwa na hazina ya mashapo ya tani milioni 40 -50 ya makaa ya mawe wakati Ivogo ina mashapo ya tani milioni 35” Alifafanua kitaalam Mhandisi Komba.

Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Ileje mkoani Songwe Bi. Mary Marco ameiomba Bodi ya STAMICO kuharakisha hatua za ufufuaji mgodi wa uzalishaji Mkaa ya Mawe na Umeme-Kiwira ili kuinusuru mitambo inayoendelea kuharibika kwa kutotumika kwa muda mrefu.

“Mkoa wetu wa Songwe ni mkoa mpya unaotegemea mapato yatokanayo na uvunaji wa rasilimali ya makaa ya mawe ya Kiwira hivyo basi kufufuliwa kwa mgodi huu kutaisaida Wilaya ya Ileje kujiongezea mapato kupitia kodi zitakazolipwa na mgodi na hivyo kuchangia kuleta maendeleo ya wilaya na Tiafa kwa ujumla.” Bi. Mary Marco alifafanua.

Imeandaliwa na:

Koleta Njelekela-STAMICO,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz