Home » images »

STAMIGOLD yashauri Wachimbaji wadogo kubuni vyanzo vingine vya mapato

 

Meneja Mkuu wa mgodi wa Biharamulo, Mhandisi Dennis Sebugwao amekishauri kikundi cha wachimbaji wadogo Mavota Gold Mine kilichopo kijiji cha Mavota wilaya ya Biharamulo kuweka mikakati madhubuti ya kuanzisha vyanzo vingine vya fedha vitakavyo wakwamua kiuchumi badala ya kutegemea uchimbaji wa dhahabu pekee.

Sebugwao alitoa ushauri huo baada ya Mwenyekiti wa kikundi hicho Pascal Joachim kuwasilisha taarifa ya kiutendaji kupitia kikao baina yao na uongozi wa mgodi kilichofanyika hivi karibuni hapa mgodini.

Kupitia kikao hicho, wanakikundi waliomba kufanya uchimbaji katika moja ya maeneo ya mgodi yaliyofanyiwa utafiti au kupewa kifusi kilichokwisha chenjuliwa maarufu kama magwangala.

“Mgodi tayari umeiomba serikali fedha kwa ajili ya utafiti, endapo zitapatikana  tutafanya utafiti katika maeneo zaidi na kubainisha yale tusiyo yahitaji ili muweze kuyaombea leseni. Vilevile mgodi huu ni mali ya serikali hatuna mamlaka ya kugawa eneo kwa mtu yeyote bila kufuata utaratibu kwani tunaweza kuleta migongano isiyo ya lazima”. Alisema Sebugwao.

Aidha, Subugwao alishauri kikundi kubuni vyanzo vingine vya fedha vitakavyo wakwamua kiuchumi badala ya kuendelea kusubiri kujikwamua kupitia uchimbaji wa dhahabu pekee ambao hutumia gharama kubwa jambo lililoungwa mkono na wanakikundi wote.

“Mfano mnaweza kutafuta zabuni hapa mgodini mathalani kuuza nafaka kama walivyofanya Kikundi cha Kina Mama Maendeleo Mavota ambao mpaka sasa wameshajipatia takribani shilingi milioni 300 kutokana na mauzo ya bidhaa mbalimbali hapa mgodini. Sioni sababu ya wafanyakazi na wakandarasi wetu kwenda Runzewe na Kahama kutafuta mahitaji yao badala ya kuyapata yote  kijijini Mavota ili waache kiasi cha fedha zao  kwa nyie mlio jirani na mgodi huu na sio kwa watu wa mbali na mgodi.” Alisisitiza Sebugwao.

Kwa upande mwingine mmoja wa wanakikundi, Ekarist Kapela aliushukuru uongozi wa mgodi kwa kuwashauri vyema hususani kutumia Shirika la Madini la Taifa STAMICO kupata maeneo yake yaliyobaki baada ya kufanyiwa utafiti ili kupunguza gharama kubwa za  uchorongaji  na pia kuepuka njia za mkato katika uchimbaji dhahabu kwani huweza kusababisha hasara kubwa.

“Kwa niaba ya kikundi naushukuru uongozi wa mgodi kwa ushauri ambao mmekuwa mkitupatia tunaomba msichoke kutusaidia pia tunawaahidi tutalifanyia kazi pendekezo la Meneja Mkuu la kujikwamua kiuchumi vilevile tutaendelea kusaidia kutoa taarifa tukiona au kusikia hali yoyote ya kutishia ulinzi au usalama katika mgodi wa Biharamulo” Alisema Kapela

Mgodi wa Biharamulo kwa nyakati tofauti umekuwa ukitoa ushauri  kwa vikundi vya wachimbaji wadogo kuhusiana namna bora ya kuendesha shughuli za uchimbaji dhahabu. Mgodi tangu kuanzishwa kwake mwaka 2014 umekuwa ukizisaida jamii  hususani za jirani na mgodi kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya afya, elimu, miundo mbinu pamoja na kutoa fursa za kibiashara kwa vikundi vitatu kutoka vijiji vya Mavota na Mkukwa na kutoa ajira za muda mfupi kwa wakazi wa vijiji hivyo.

Imeandaliwa na:

Jacqueline Mattowo,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz