Taarifa kwa Umma-Ajali ya wachimbaji wadogo wapatao 18 kufukiwa na kifusi baada ya shimo kuporomoka

 

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA NISHATI NA MADINI

 TAARIFA KWA UMMA

AJALI YA WACHIMBAJI WADOGO WAPATAO 18 KUFUKIWA NA KIFUSI BAADA YA SHIMO KUPOROMOKA KATIKA ENEO LENYE LESENI YA UTAFUTAJI MADINI NA. PL 7132/2011 INAYOMILIKIWA NA STAMICO

Wizara ya Nishati na Madini inapenda kuufahamisha umma kuwa, Tarehe 13 Februari, 2017 kulitokea ajali ya wachimbaji wadogo wapatao 18 kufukiwa na kifusi wakati wakichimba dhahabu katika eneo la Buhemba lenye leseni ya utafutaji wa madini ya dhahabu, PL No. 7132/2011 inayomilikiwa na STAMICO. Ajali hiyo ilitokana na kuporomoka kwa mwamba wakati wachimbaji hao walipovamia eneo hilo na kuanza kuchimba dhahabu kitendo ambacho kimekuwa kikifanyika hasa wakati wa usiku.

Wachimbaji 13 waliokolewa tarehe hiyo hiyo 13 Februari, 2017 wakiwa hai na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama kwa matibabu. Zoezi la kutafuta wachimbaji wengine liliendelea ambapo tarehe 14 Februari, 2017 maiti mbili zilipatikana katika shimo hilo. Juhudi zaidi zinaendelea kutafuta wachimbaji wengine waliobaki ambapo Uongozi wa Wilaya ya Musoma kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Wizara ya Nishati na Madini kupitia Ofisi ya Madini Musoma kwa kushirikiana na  Mgodi wa North Mara na Wachimbaji wadogo wanaendelea na  zoezi la uokoaji. Juhudi za kufukua shimo lililoporomoka pia zinaendelea ili kuona kama kuna watu zaidi katika shimo hilo. Mgodi wa North Mara umetoa msaada wa mashine ya kuvuta maji na tope ili kuwezesha zoezi la ufukuaji kuendelea.

Wizara ya Nishati na Madini inachukua fursa hii kuwatangazia Wananchi wote kuwa shughuli za Utafutaji, Uchimbaji na biashara au shughuli yoyote ya madini  zinatakiwa zifanyike kwa kuzingatia Sheria ya Madini ya Mwaka 2010. Kwa maana hiyo, lazima shughuli hizo zifanywe na wamiliki wa leseni na vibali halali vinavyotolewa kwa mujibu wa sheria hiyo. Kwa kufanya hivyo, itawezesha wataalam wa Wizara ya Nishati na madini kufanya ukaguzi ili kuhakikisha kuwa shughuli hizo zinafanyika inavyotakiwa ikiwa ni pamoja na usalama katika shughuli za uchimbaji.

Tunatoa wito kwa Wananchi wote ikiwa ni pamoja na wachimbaji wadogo kuacha tabia ya kuvamia maeneo na kuendesha uchimbaji katika eneo lolote bila kumiliki leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

 

Imetolewa na;

KATIBU MKUU

WIZARA YA NISHATI NA MADINI