Taarifa kwa umma kuhusu ukusanyaji madeni ya umeme

 

  SHIRIKA LA UMEME TANZANIATAARIFA KWA UMMA KUHUSU UKUSANYAJI MADENI YA UMEME

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linautaarifu umma na wateja wake wote kwa ujumla kuwa, linakusudia kuendesha Zoezi kabambe la ukusanyaji wa madeni ya bili za Umeme zilizolimbikizwa na wateja mbalimbali wa Shirika Nchi nzima. Madeni hayo yanajumuisha madeni ya wateja wadogo, Wizara, Taasisi za mbalimbali za Serikali pamoja na Makampuni binafsi.

Malimbikizo hayo ya madeni yamekuwa yakikwamisha jitihada za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya msingi ndani ya Shirika kwa wakati ikiwemo shughuli za Uendeshaji Shirika, Matengenezo ya Miundombinu pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Zoezi hili litaambatana na utoaji taarifa (notice) kwa wadaiwa wote kulipa madeni yao ndani ya kipindi cha siku 14, baada ya hapo Shirika litachukua hatua ya kusitisha Huduma kwa Wateja watakaoshindwa kuanza kulipa madeni yao pamoja na hatua zingine za kisheria.

Aidha, hadi kufikia kipindi cha Januari, 2017, Shirika linawadai Wateja wake wote jumla ya shilingi 275,381,708,253.66. Deni la Wizara na Taasisi za Serikali  ni Tshs. 52,534,910,207.22, Makampuni binafsi na wateja wadogo ni 94,973,062,736.94 pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ambalo linadaiwa jumla ya Tshs. 127,873,735,309.50

Ni matarajio ya Shirika kuwa kulipwa kwa malimbikizo haya ya madeni, kutasaidia TANESCO kujiendesha kiushindani na kwa ufanisi mkubwa zaidi na hivyo kuendelea kuchochea kasi ya ukuaji sekta mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme hapa Nchini.

IMETOLEWA NA:  SHIRIKA LA UMEME TANZANIA (TANESCO)