Taarifa kwa Umma-Kukanusha taarifa zinazoenezwa na Kampuni ya Dangote na washirika wake

 

SHIRIKA LA MAENDELEO YA PETROLI TANZANIA (TPDC)

tpdc

TAARIFA KWA UMMA

Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) linapenda kukanusha taarifa zinazoenezwa na Kampuni ya Dangote pamoja na washirika wake kupitia mitandao ya kijamii, pamoja na vyombo vya habari vikidai kuwa TPDC imeshindwa kukiuzia gesi asilia kwa bei rahisi Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mkoani Mtwara na hivyo kuwa moja ya sababu ya kusimamisha uzalishaji wa kiwanda hicho.

TPDC inapenda kutoa taarifa kwamba imefanya jitahada mbalimbali kuhakikisha kwamba Kampuni ya Dangote inapata nishati hiyo muhimu kwa ajili ya kuzalisha saruji, ikiwemo kufanyika kwa vikao mbalimbali, pamoja na makubaliano yaliyofanyika kwa Dangote kuridhia nia yao ya kutumia gesi asilia kuzalisha umeme kwa ajili ya Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara

TPDC hufuata kanuni na utaratibu wa kupanga bei ya gesi asilia ambapo hupanga kulingana na aina ya mteja. Wateja wamegawanyika kufuatia makundi tofauti kama vile wateja wa viwandani, majumbani, magari pamoja na wateja wa kuzalisha umeme. Hata hivyo bei elekezi ambayo inakua inapendekezwa na TPDC lazima iridhiwe na ipitishwe na EWURA ndipo ianze kutumika.

Dangote kama mtumiaji wa matumizi ya viwandani amekuwa na mazungumzo ya muda mrefu na TPDC kuhusu bei ya gesi asilia. Kiwanda cha Dangote kimeomba kupewa gesi asilia kwa bei ambayo hapa kwetu Tanzania ni kidogo kwani kiasi hicho cha bei ndicho kinacholipwa kununulia gesi ghafi kutoka kisimani. Gesi ghafi kutoka kisimani hupitishwa kwenye mitambo ya kuchakata gesi asilia ili kufikia viwango vinavyokubalika kwa mtumiaji na baadaye kusafirishwa kupitia bomba kwenda kwa mtumiaji. Hivyo basi, TPDC haiwezi kuuza gesi asilia kwa bei ya kisimani kwa sababu kuna gharama zinazoongezeka katika kuisafisha na kuisafirisha gesi hiyo.

TPDC imefanya majadiliano ya mkataba ya awali na Kiwanda cha Saruji cha Dangote kwa ajili ya kuwauzia gesi asilia itakayotumika kuzalishia umeme utakaotumiwa na kiwanda hicho. Inategemewa hadi kufikia mwezi Januari 2016 miundombinu ya gesi asilia itakua imeshaunganishwa na mitambo ya kufua umeme utakaotumiwa na Kiwanda hicho.

TPDC ni Shirika la Mafuta la Taifa linalofanya kazi zake kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi, na kuwajali wawekezaji akiwemo Dangote ili wawekeze katika kukuza uchumi wa nchi.

Hivyo si sahihi kusema TPDC imemkwamisha Dangote katika uzalishaji wa Saruji Mkoani Mtwara. Taarifa hizi hazina mantiki yoyote na zinapswa kupuuzwa kwani TPDC imefanya jitihada kuhahikisha kwamba kampuni ya Dangote inaendelea na uzalishaji wa saruji kama ilivyokusudiwa.

 

Imetolewa na:
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania

 

 

TPDC kwa maendeleo ya Taifa”