Home » Latest »

Taarifa kwa vyombo vya habari-Serikali yaridhia utekelezaji wa ujenzi wa bomba la mafuta

 

Serikali ya Tanzania imeridhia rasmi utekelezaji wa mradi ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Kabaale katika Wilaya ya Hoima nchini Uganda hadi bandariya Tanga nchini Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, akiongoza Baraza la Mawaziri Ikulu jijini Dar es Salaam, September 29,2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, akiongoza Baraza la Mawaziri Ikulu jijini Dar es Salaam, September 29,2016.

Uamuzi huo umefikiwa katika Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika leo (tarehe 29 Septemba, 2016) Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Taarifa ya kuridhiwa rasmi kwa mradi huo imetolewa naWaziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ambaye amesema ujenzi wa mradi huo utakaoanza wakati wowote kuanzia sasa unatarajiwa kukamilika mwaka 2020.

Amesema ujenzi wa bomba hilo unatarajiwa kugharimu dola za Marekani Bilioni 3.5 ambapo kati yake Dola Bilioni 3 zitatumika kujenga bomba upande wa Tanzania.

Mradi huo mkubwa utatekelezwa kwa ubia wa ujenzi na uendeshaji kwa kushirikishaka mpuni za Total ya Ufaransa, CNOOC ya China, Tullow ya Uingereza na Serikali za Tanzania na Uganda.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa taarifa juu ya maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu Serikali kuridhia utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Kabaale katika Wilaya ya Hoima nchini Uganda, hadi Bandari ya Tanga.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa taarifa juu ya maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu Serikali kuridhia utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta kutoka Kabaale katika Wilaya ya Hoima nchini Uganda, hadi Bandari ya Tanga.

Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa bomba hilo lenye urefu wa kilometa 1,443 linatarajiwa kusafirisha mapipa 200,000 kwa siku ambapo kila pipa litaliingizia taifa Dola za Marekani 12.2.

Amebainisha kuwa pamoja na kusafirisha mafuta ya kutoka nchini Uganda bomba hilo pia linatarajiwa kusafirisha mafuta kutoka nchi nyingine za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sudani Kusini ambazo zimeonesha nia ya  kusafirisha mafuta yao kupitia bandari ya Tanga.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametaja faida nyingine ambazo Tanzania itazipata kutokana na mradi huo kuwa ni kupatikana kwa ajira zaidi ya 15,000 wakati wa ujenzi na ajira 2,000 baada ya ujenzi kukamilika, kuimarika kwa mahusiano ya kidiplomasia, kukuza biashara katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania, kampuni za ujenzi za Tanzania kupata kazi za ujenzi.

Aidha, amesema Tanzania inatarajia kunufaika zaidi kwa kutumia bomba hilo kupitisha mafuta yanayotarajiwa kupatikana katika maeneo ya ziwa Tanganyika na Ziwa Eyasi.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM
ALHAMIS, SEPTEMBA  29, 2016