Home » images »

TANESCO yatakiwa kukagua mitambo yake

 

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetakiwa kuhakikisha linafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mitambo ya kuzalisha umeme ili kuepuka kuharibika ama kushuka kwa utendaji wake na hivyo kusababisha usumbufu kwa wananchi wa kukatika katika kwa umeme.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kulia) akikagua Kituo cha Kufua umeme kwa kutumia mafuta mazito (HFO) cha Megawati 60 cha Nyakato Jijini Mwanza. Kushoto ni Meneja wa kituo hicho, Mhandisi Mathew Mwangomba.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alipofanya ziara kwenye Kituo cha Kufua Umeme kwa kutumia mafuta mazito cha Megawati 60 cha Nyakato jijini Mwanza ili kujionea  hali ya mitambo kwenye kituo hicho.

Aliagiza suala la kusubiri miezi sita ndiyo kufanya ukaguzi lisiendelee na kuwa ukaguzi ufanyike kila mwezi na ikibidi hata kila wiki kuwe na ukaguzi wa mitambo husika ili ifanye kazi kwa ufanisi unaotakiwa.

Dkt. Kalemani alisema ziara hiyo inafuatia kikao cha Desemba 19, 2016 baina ya Serikali na Wakandarasi ambao ni Kampuni ya SEMCO Maritime As ya Denmark na Rolls-Royce As ya Norway kilichojadili kuhusiana na hitilafu iliyotokea kwa mitambo minne ambayo imesimama kuzalisha umeme.

Alisema ni muda mfupi mitambo imefanya kazi tangu kukamilika ujenzi wake. “Hatuwezi kukubali hali ya namna hii iendelee kwani kituo kilianza rasmi kazi mwaka 2013 halafu sasa hivi, mitambo minne haifanyi kazi; ni lazima majadiliano yafike mwisho na yawe katika maandishi; tuhakikishe mitambo inafanya kazi,” alisema Dkt Kalemani.

Alisema kituo hicho kinayo jumla ya mitambo 10 ambayo kwa pamoja ina uwezo wa kuzalisha megawati 60 huku kila mtambo ukizalisha megawati sita lakini kutokana na hitilafu ya mitambo minne, hivi sasa megawati zinazozalishwa ni 36 pekee.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akielekeza jambo wakati wa ziara ya kukagua mitambo ya kuzalisha umeme ya Nyakato Jijini Mwanza. Kulia ni Meneja wa Mitambo, Mhandisi Mathew Mwangomba.

“Hizi megawati zinazozalishwa hivi sasa ni kidogo, ni lazima tuhakikishe Kituo kinazalisha kama ilivyokusudiwa hata kama kwa sasa hakuna mahitaji hayo kwa hapa Mwanza,” alisema.

Aidha, Naibu Waziri Kalemani alimuagiza Meneja wa TANESCO, Mkoa wa Mwanza kuhakikisha anatembelea maeneo yote yenye kero za kukatika kwa umeme mkoani humo na ashughulikie hasa ikizingatiwa umeme unaofika mkoani humo unatosheleza na kwamba suala hilo halina mjadala.

Dkt. Kalemani alibainisha kuwa atafanya ziara kote kwenye vituo vya kufua umeme nchini ili kujionea hali na ufanisi wake pamoja na kubaini hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Serikali mara baada ya ziara katika maeneo hayo.

 

Imeandaliwa na:

Mohamed Saif,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz