Uchimbaji gesi ya helium kuanza baada ya utafiti wa kina

 

Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa uchimbaji wa gesi ya Helium utaanza mara baada ya kazi ya utafiti wa kina, upembuzi yakinifu na tathmini ya athari za mazingira kukamilika.

Aliongeza kuwa, lengo ni kubaini kiasi halisi cha gesi kitakachopatikana na leseni ya uchimbaji kutolewa na kuongeza kuwa, uchorongaji unatarajiwa kuanza mwaka 2018.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo Bungeni mjini Dodoma, tarehe 4 Machi, 2017 wakati akijibu swali la Mbunge wa Kwela, Ignas Malocha aliyetaka kujua ni lini Serikali itaanza kuchimba gesi hiyo ili watanzania waanze kunufaika na gesi hiyo kabla haijagunduliwa na kuchimbwa mahali pengine duniani.

Naibu Waziri alieleza kuwa, ni kweli kwamba Kampuni ya Helium One Limited imefanya utafiti wa gesi ya Helium katika bonde la Ziwa Rukwa, ambapo taarifa za awali zinaonyesha uwezekano wa kuwapo kwa gesi ya Helium kiasi cha futi za ujazo bilioni 54 katika maeneo ya ziwa Rukwa.

“Matokeo haya yanatokana na uchunguzi wa sampuli tano za mavujia (Gas Seeps) ya gesi ya Helium katika maeneo hayo, kiasi ambacho kinakadiriwa kuwa kikubwa zaidi ya mara sita ya mahitaji ya dunia kwa sasa,” alisema Dkt. Kalemani.

Aliongeza kuwa, Kampuni ya Helium One Limited imefanya utafiti huo kupitia Kampuni zake tanzu za Gogota (TZ) Limited, Njozi (TZ) Limited na Stahamili (TZ) Limited zinazomiliki leseni za utafutaji wa gesi ya Helium katika Mkoa wa Rukwa ikiwemo maeneo ya ziwa Rukwa.

“Mheshimiwa Spika, Shughuli za utafutaji wa kina wa gesi ya Helium unaendelea kwa kukusanya taarifa zaidi za kijiolojia, kijiokemia, kijiofizikia na 2D Seismic survey ili zitumike kwa ajili ya uchorongaji wa visima vya utafiti (Exploratory well).

Gesi hiyo adimu hutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuendesha mashine za utabibu zijulikanazo kama MRI scanners, mbali na kutumika katika mitambo ya kinyuklia, Helium hutumika kwenye unajimu, Helium pia hutumika kujaza maputo ya sherehe, hutumiwa na wapiga mbizi na wengine wanaofanya kazi kwenye hewa nzito na hutumika kubaini alama kwenye maduka makubwa (barcodes).

Imeandaliwa na:

Asteria Muhozya,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz