Utekelezaji bomba la mafuta safi Tanzania-Zambia

 
  • KAMATI YAANZA KAZI

Tarehe 20 hadi 22 Februari 2017, ulifanyika Mkutano wa Kwanza wa Kamati ya Kusimamia utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta safi litakaloanzia Dar es Salaam, Tanzania hadi Ndola, Zambia.

Mkutano huo wa Kamati ambayo imepewa jina la New TAZAMA Products Pipeline Project Inter-governmental Committee ulifanyika katika kituo cha kusukuma Mafuta cha TAZAMA kilichopo katika mji wa Chinsali, Zambia.

Mkutano uliongozwa na Brigedia Jenerali Mstaafu Emelda Chola, Katibu Mkuu wa Nishati (Wizara ya Nishati Zambia) na kuhudhuriwa na Wizara pamoja na taasisi za Serikali za nchi zote mbili huku  Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Prof. Justin Ntalikwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.

Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Safi (White Petroleum Product) kutoka Dar es Salaam Tanzania hadi Ndola-Zambia utahusisha ujenzi wa Bomba lenye urefu wa takribani kilomita 1710 litakalojengwa sambamba na Bomba la TAZAMA linalosafirisha mafuta yasiyosafishwa (Crude Oil) kutoka Dar es Salaam, hadi Ndola Zambia.

Mradi huu pia utahusisha ujenzi wa  matoleo  ya mafuta (take-off points) katika maeneo ya Chalinze, Morogoro, Makambako, Mbeya na Songwe ambayo yatatumika kusambaza mafuta kwa mikoa ya kanda za kaskazini, Kati, kusini na Nyanda za juu.

Makubaliano ya kuanza ujenzi wa Bomba la kusafirisha Mafuta Safi yalitokana na Ziara ya  Rais wa Jamhuri ya Zambia Mhe. Edgar Chagwa Lungu, aliyoifanya nchini Tanzania tarehe 29 Novemba, 2016 na kukutana na  Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph   Magufuli.

Bomba hili litajengwa kwa ushirikiano wa nchi hizi mbili Tanzania na Zambia na utaleta manufaa makubwa kwa nchi zote.

Kwa upande wa Tanzania manufaa yatakayopatikana ni pamoja na uhakika wa usafirishaji usambazaji na upatikanaji, wa mafuta nchini;  bei nafuu katika kusafirisha mafuta ikiwa pamoja na kupunguza matumizi ya malori ya mafuta ambayo yamekuwa yakiharibu miundombinu ya barabara.

Aidha, mradi huu utarahisisha upatikanaji wa mafuta kwa mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Ruvuma, Iringa, Mbeya, Sumbawanga, Mpanda na Kigoma. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuanza Mwaka 2018 na kukamilika Mwaka 2021.

Imeandaliwa na:

Teresia Mhagama,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz