Home » images »

Utekelezaji REA iIi kushirikisha Viongozi

 

Wakandarasi watakaotekeleza Miradi ya Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) wametakiwa kuhakikisha wanashirikisha viongozi wa maeneo husika kabla ya kuanza utekelezaji wake.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kulia) alipotembelea mgodi wa dhahabu wa Musasa uliopo wilayani Chato na kuzungumza na wachimbaji juu ya masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa REA III. Mwenye kipaza sauti ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaban Ntarambe.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni kwa nyakati tofauti Wilayani Chato na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara na wananchi wa wilaya hiyo na alipofanya ziara kwenye machimbo ya dhahabu ya Musasa.

Dkt. Kalemani alisema kila Mkandarasi anapaswa kabla hajaanza kutekeleza mradi husika ashirikiane na viongozi wa maeneo yanayopelekewa mradi ili kuharakisha utekelezaji wake na kuepusha migonagano isiyokuwa na tija.

Alisema kwa wilaya hiyo ya Chato, Mradi wa REA III utaanza kutekelezwa rasmi ifikapo mwezi Machi 25, 2017 na hivyo aliwaasa wananchi kuhakikisha wanachangamkia fursa hiyo ili kujiletea maendeleo.

“Mradi huu wa REA Awamu ya Tatu ni wa miaka minne, na ninawakumbusha kwamba huduma ya umeme ni ya lazima; kwahiyo changamkieni,” alisema Dkt. Kalemani.

Alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, alisema kila mwananchi anayo haki ya kuunganishwa na huduma ya umeme na hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuchangamkia kuunganishiwa huduma kwa gharama ya shilingi 27,000.

Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Chato wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani).

Aidha, alipokutana na wachimbaji wadogo wa machimbo ya dhahabu ya Musasa yaliyopo kwenye Kata ya Makurugusi, Dkt. Kalemani alisema ili kuwa na uchimbaji wenye tija, huduma ya umeme haikwepeki.

Alisema mgodi unazo shughuli nyingi zenye kuhitaji huduma ya nishati ya umeme na hivyo kwa kutambua hilo, Serikali itahakikisha huduma hiyo inafika kama ilivyokusudiwa.

Aliongeza kwamba umeme unahitajika kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kuendeshea mitambo ya kuchenjulia dhahabu pamoja na pampu za kuvutia maji kwenye mashimo pale yatakapokuwa yamejaa maji hususan kipindi cha masika  na ambayo vilevile itasaidia kupunguza ajali.

“Ukitumia umeme kwenye kuchimba, unapunguza nguvu kubwa ya kuwekeza na unapata mapato makubwa na faida kubwa,” alisema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani alifafanua kwamba mbali na matumizi ya umeme katika shughuli za uchimbaji, huduma hiyo ya umeme vilevile inahitajika kwa wananchi ambao wanajishughulisha na biashara mbalimbali ikiwemo ya migahawa.

Imeandaliwa na:

Mohamed Saif,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz