Home » images »

Uwekaji jiwe la msingi mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga, Tanzania

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, tarehe 5 Agosti, 2017, waliweka jiwe la Msingi la Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni wakiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Serikali ya Tanzania iliyoshiriki wakati wa majadiliano ya mradi husika.

Sherehe za uwekaji jiwe la msingi zilifanyika katika eneo la Chongoleani eneo itakapojengwa gati ya kushusha mafuta jijini Tanga na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa, Vyama vya Kisiasa, Viongozi wa dini, Ujumbe Maalum kutoka Serikali ya Uganda, Taasisi Binafsi, Wawakilishi kutoka Taasisi mbalimbali za umma, Balozi za nje nchini, Taasisi za Kimataifa, wabunge wanaotoka maeneo ambayo bomba litapita, Wawakilishi kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Wakuu wa Mikoa ambayo Bomba litapita, Wakuu wa Wilaya ambao bomba litapita, Wakuu wa Mikoa jirani na jiji la Tanga, Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi wa Mkoa wa Tanga na wananchi  wengine.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli (kulia) na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni (kushoto) wakipongezana baada ya kuweka jiwe la Msingi la Mradi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga- Tanzania.

Mradi huo mkubwa utatekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali za Uganda na Tanzania na pia utahusisha kampuni za TOTAL E & P ya Ufaransa, TULLOW Oil ya Uingereza na China National Offshore Oil Corporation (CNOOC) ya China.

Bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,445 kutoka Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga Tanzania. Kati ya kilomita hizo, kilometa 1,149 zitajengwa ndani ya ardhi ya Tanzania na mradi utagharimu jumla ya Dola za Marekani Bilioni 3.55. Aidha, bomba hilo litasafirisha mapipa kati ya laki mbili (200,000) na laki mbili na kumi na sita elfu (210,000) kwa siku.

 Imeandaliwa na:

Asteria Muhozya,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

Barua Pepe: info@mem.go.tz,                                                                               

Tovuti: mem.go.tz