Wachimbaji jiungeni katika vikundi-Dkt. Kalemani

 

Wachimbaji wadogo wa madini nchini wamekumbushwa kujiunga katika vikundi na kuvisajili kisheria ili iwe rahisi kuwezeshwa na hivyo kuwa na uchimbaji wenye tija.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa tatu kulia) alipotembelea machimbo ya dhahabu ya Musasa, wilayani Chato. Nyuma yake ni Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi, Mhandisi Yahaya Samamba

Wito huo umetolewa hivi karibuni na Naibu waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani alipofanya ziara kwenye mgodi wa dhahabu wa Musasa uliopo Wilayani Chato na kuzungumza na wachimbaji.

Dkt. Kalemani alielezea umuhimu wa kujiunga katika vikundi na kusajiliwa ikiwemo urahisi wa kupata huduma za kifedha na kukopesheka, kuelimishwa njia bora ya uchimbaji na vilevile urahisi wa kupatiwa ruzuku.

Aliongeza kuwa endapo kama mchimbaji ama wachimbaji watashindwa kuendeleza eneo walilokatia leseni ni vyema wakatafuta wabia ili kuongeza nguvu ya kufanya shughuli husika.

“Kama hamuwezi kuchimba ingieni ubia, mtatoka kwenye uchimbaji mdogo kwenda wa kati na baadaye kuwa mkubwa; msiogope jiungeni kwenye vikundi msajiliwe mpeane nguvu mfanye vizuri zaidi,” alisema.

Alisema wachimbaji hao watakapojiunga, wataweza kuwa na uchimbaji wenye tija na hivyo kutoa ajira nyingi, kulipa ushuru na tozo mbalimbali na hivyo kujiletea maendeleo wao binafsi lakini pia maendeleo kwa Taifa kwa ujumla.

Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Ziwa Viktoria Magharibi, Mhandisi Yahaya Samamba (kulia) akizungumzia masuala ya uchimbaji wa madini wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kushoto) katika machimbo ya dhahabu ya Musasa yaliyopo wilayani Chato.

Aidha, aliwaeleza kuwa taratibu za kujiunga zikikamilika, ni vyema wakawa na Meneja ambaye atasimamia shughuli mbalimbali za uchimbaji ikiwemo kusimamia suala la ajira, usalama na mazingira kwenye machimbo husika.

“Mkiwa na Meneja mtapunguza migogoro mbalimbali ikiwemo ya ajira na hata ajali kwani miongoni mwa majukumu yake ni pamoja na kushughulikia masuala husika,” alisema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani vilevile alionya ajira za watoto migodini na kueleza kwamba kuwatumikisha ni kosa kisheria na hivyo endapo kuna mchimbaji anaefanya hivyo aache mara moja.

Imeandaliwa na:

Mohamed Saif,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz