Home » images »

Wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini na Mbunge wa Simanjiro wafanya ziara katika Maduka ya Tanzanite, Arusha

 

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na Mbunge wa Simanjiro, Mhe.James Millya, wametembelea baadhi ya maduka  yanayouza madini ya Tanzanite jijini Arusha ili kujionea shughuli za biashara na uongezaji thamani wa madini hayo zinavyofanyika.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini (CHADEMA),(wa pili kulia), Mhe. Mwantakaje Juma Mbunge wa Bububu (CCM) (wa pili kushoto) na Mbunge wa Simanjiro, Mhe. James Millya (wa kwanza kulia) wakiwa ndani ya Mgodi wa mfano wa Tanzanite uliopo ndani ya duka la The Tanzanite Experience jijini Arusha. Mgodi huo hutumika kutoa elimu kwa wageni mbalimbali kuhusu shughuli za uchimbaji wa Tanzanite. Wa kwanza kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Kaskazini, Adam Juma.

Ziara hiyo ni moja ya majukumu waliyopanga kuyafanya jijini Arusha, jukumu kuu likiwa ni kushuhudia jinsi Mnada wa Pili wa Kimataifa wa Madini ya Tanzanite unavyofanyika katika kituo cha Jemolojia jijini Arusha.

Moja ya duka lililotembelewa na Wabunge hao ni The Tanzanite Experience ambalo hujishughulisha na kukata Tanzanite ili kuiweka katika maumbo mbalimbali na kuing’arisha.

Mbunge wa Simanjiro, Mhe. James Millya (wa nne kulia) na Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Kitandula, Mbunge wa Mkinga (CCM), (wa pili kulia), Mhe. Mwantakaje Juma Mbunge wa Bububu (CCM) (wa Tatu kulia) na wakipata maelezo kuhusu biashara ya Tanzanite ndani ya duka la The Tanzanite Experience jijini Arusha. Anayetoa maelezo ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Hasnain Sajan. Wa kwanza kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Madini, Kanda ya Kaskazini, Adam Juma.

Duka la The Tanzanite Experience pia hutoa elimu bure kwa wanafunzi na wageni mbalimbali kuhusu madini ya Tanzanite ikiwemo historia yake.

Ndani ya duka hilo pia kumejengwa  mgodi wa mfano wa Tanzanite ambao hutumika kutoa elimu kwa wageni mbalimbali kuhusu shughuli za uchimbaji wa Tanzanite.

Baadhi ya Wajumbe waliofanya ziara hiyo ni pamoja na Mhe. John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini (CHADEMA), Mhe. Mwantakaje Juma Mbunge wa Bububu (CCM) na Mhe. Dunstan  Kitandula Mbunge wa Mkinga (CCM).

Imeandaliwa na:

Teresia Mhagama,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz