Home » images »

Wanawake 47 wahitimu mafunzo ya ukataji na ung’arishaji Vito

 

Imeelezwa kuwa jumla ya wanawake 47  wamehitimu mafunzo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito yanayotolewa na Kituo cha Jemolojia jijini Arusha ambacho kipo chini ya Wizara ya Nishati na Madini.

Mkufunzi Msaidizi katika Kituo cha Jemolojia Arusha, (TGC), Lilian Petro (wa kwanza kulia) akionyesha madini ya vito yaliyong’arishwa na wanafunzi wanaopata mafunzo katika Kituo hicho kilicho chini ya Wizara ya Nishati na Madini. Wa Pili kulia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Uthamini wa Madini ya Almasi na Vito (TANSORT), Archard Kalugendo, wa Pili kushoto ni Mhe. Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum (CCM) na wa kwanza kushoto ni Beatrice Lupi, Mhasibu Mkuu kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).

Hayo yalisemwa jijini Arusha na Kaimu Mratibu wa Kituo hicho, Erick Mpesa wakati wa Mnada wa Pili wa Kimataifa wa Madini ya Tanzanite unaofanyika jijini Arusha katika Kituo hicho.

Mpesa alisema kuwa mafunzo hayo yalianza kutolewa mwaka 2014 ambapo katika Awamu ya kwanza wanafunzi 15 walihitimu, Awamu ya Pili walihitimu  wanafunzi 14 na Awamu ya Tatu walihitimu wanafunzi 18.

“Mafunzo haya hutolewa kwa muda wa miezi Saba  ambapo Wanafunzi hawa ambao huwa na  umri wa chini ya miaka 30 wanafadhiliwa na Mfuko wa Kuwaendeleza Wanawake chini ya Kamati ya Maonesho ya Vito ya Arusha (AGF) na Wizara ya Nishati na Madini,” alisema Mpesa.

Mratibu wa TGC aliongeza kuwa Kituo hicho  pia kinaendesha shughuli  za uchongaji wa mawe ya miamba kwa kutengeneza vinyago vyenye maumbo mbalimbali kama ya wanyama, ndege, samaki na vitu mbalimbali vya urembo.

Samadu Mohamed, kutoka Kituo cha Jemolojia Arusha, akionesha moja ya vinyago vinavyotokana na mawe ya miamba vinavyotengenezwa katika kituo hicho.

Akizungumzia mafanikio ya kituo hicho, Mpesa alisema kuwa mbali ya kusaidia wanawake hao kupata mafunzo yatakayowasaida kujiajiri au kuajiriwa, Kituo hicho  ni cha pekee Afrika Mashariki kinachoendeleza taaluma ya uongezaji thamani madini ya vito na miamba.

Mmoja wa wanafunzi katika Kituo cha Jemolojia Arusha, Zuwena Mtoo, akionesha utaalam wa kukata na kung’arisha madini ya Vito, baada ya kupata mafunzo katika Kituo hicho kilicho chini ya Wizara ya Nishati na Madini.

Kuhusu mipango ya kuendeleza Chuo hicho alisema kuwa, Chuo kimepanga kutoa mafunzo ya muda mrefu kwa ngazi ya diploma ambapo mitaala ya kozi mbalimbali za taaluma ya vito na usonara imeandaliwa na kuwasilishwa katika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ambapo mchakato wa ithibati na usajili unaendelea.

Kwa  upande wake Mkufunzi Msaidizi wa TGC, Lilian Petro, alisema kuwa mafunzo hayo husaidia wanafunzi hao kutambua madini ya aina mbalimbali, kuyakata na kufahamu thamani ya madini husika.

Aidha Lilian, Alitoa ushauri kwa wanawake mbalimbali nchini kujiunga katika fani hiyo ya ukataji na ung’arishaji wa madini ya vito kwa kuwa inamsaidia mtu kujiajiri kwa kuanzisha vituo vya ung’arishaji wa madini ya vito ndani ya nchi na pia kuajiriwa.

Imeandaliwa na:

Zuena Msuya,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz