Home » images »

Waziri Muhongo akutana na kampuni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia nchini

 

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema mikutano ya kila baada ya miezi mitatu na Kampuni zinazojihusisha na Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Nchini itakuwa ikifanyika katika maeneo mbalimbali nchini hususan kwenye rasilimali husika.

Baadhi ya wawakilishi wa Kampuni za Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Nchini kwenye mkutano na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).

Waziri Muhongo aliyasema hayo hivi karibuni Mkoani Mtwara wakati wa mkutano wake na wawakilishi wa kampuni hizo uliofanyikia kwenye Kituo cha Kuchakata Gesi Asilia cha Madimba.

Alisema mikutano husika ilikua ikifanyikia jijini Dar es Salaam lakini ili kuleta tija zaidi, imeamuliwa iwe inafanyikia kwenye maeneo yenye gesi asilia na baadaye siku za usoni itafanyika kwenye maeneo yatakayogundulika kuwa na mafuta.

Baadhi ya wawakilishi wa Kampuni za Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Nchini kwenye mkutano na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).

Aliongeza kuwa kila baada ya miezi mitatu kumekuwepo na utaratibu wa kukutana kwa ajili ya kutathmini tmaendeleo ya miradi husika na kila kampuni inawasilisha ratiba yake ya kazi ambayo inajadiliwa.

“Hii mikutano kila kampuni inatupatia ratiba yake ya kazi, tunaijadili na tunashauriana na kama wana matatizo tunatafuta suluhisho,” alisema Waziri Muhongo.

Waziri Muhongo alisema shughuli za Utafutaji, Uvunaji na Uendelezaji wa Gesi Asilia na Mafuta zinaendelea vizuri huku majadiliano mbalimbali yakiendelea kuhusiana na utekelezaji wa miradi husika.

Imeandaliwa na:

Mohamed Saif,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

5 Barabara ya Samora Machel,

S.L.P 2000,

11474 Dar es Salaam,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606

Barua Pepe: info@mem.go.tz                                                                               

Tovuti: mem.go.tz