Home » images »

Waziri Muhongo awafariji wachimbaji waliopatwa maafa Sikonge

 
  • Atoa siku tatu kuchukua hatua za uchimbaji salama
  • Timu husika yakamilisha zoezi la uhakiki wa usalama

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amezuru eneo la machimbo ya madini, kulikotokea maafa ya wachimbaji saba kupoteza maisha kwa kufukiwa na kifusi na mwingine kukosa hewa, Aprili 20, mwaka huu.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), akisaini kitabu cha wageni, ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri (kushoto), kabla ya kuelekea eneo la Kitunda, wilayani Sikonge kulikotokea maafa ya wachimbaji wadogo wa madini saba baada ya kufukiwa na kifusi hivi karibuni.

Ziara ya Profesa Muhongo katika eneo hilo la machimbo yaliyopo wilayani Sikonge, mkoani Tabora, ilifanyika Mei 8 mwaka huu, ambapo ililenga kuwafariji wananchi, kuzungumza na wamiliki wa migodi pamoja na wachimbaji na kutoa mwongozo wa Serikali kuhusu hatua za kufuatwa ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji wa madini zinafanyika kwa usalama.

Akizungumza na wananchi baada ya kukagua eneo yalipotokea maafa, Profesa Muhongo alitoa muda wa siku tatu kwa Mkaguzi Mkuu wa Migodi nchini, Mhandisi Ally Samaje kwa kushirikiana na Ofisi ya Madini Kanda ya Kati-Magharibi, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Tabora pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa husika ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Aggrey Mwanri, kufanya ukaguzi na kuchukua hatua zitakazohakikisha shughuli za uchimbaji mahala hapo zinafanyika kwa usalama.

Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati-Magharibi, Salim Salim (kushoto), akitoa maelezo kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia), namna ajali iliyoua watu saba kutokana na kufukiwa na kifusi katika Mgodi unaomilikiwa na kikundi cha WINIMA, eneo la Kitunda, wilayani Sikonge mkoani Tabora, ilivyotokea.

Akifafanua zaidi kuhusu mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa na Timu hiyo ya ukaguzi, alisema ni lazima ipatikane orodha kamili ya wananchi walio tayari kufanya kazi katika migodi husika ili wajulikane, kukagua kwa kina eneo lote la migodi ili kujionea hali halisi pamoja na kutoa mwongozo/ushauri kwa wamiliki wa leseni husika kuhusu namna bora ya kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini kwa njia salama.

Akizungumza na Jarida hili mapema leo (Mei 11, 2017), Mhandisi Samaje, kwa niaba ya Timu iliyoagizwa na Waziri kushughulikia hatua za kiusalama, alisema kuwa tayari wamekamilisha kazi waliyopewa na kwamba wamewapatia mwongozo wa utendaji kazi wamiliki wa leseni husika.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri (wa pili kulia), akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini na wananchi wa eneo la Kitunda kulikotokea maafa ya watu saba baada ya kufukiwa na kifusi, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kulia) hivi karibuni. Wa tatu kutoka kulia ni Mkaguzi Mkuu wa Migodi nchini, Mhandisi Ally Samaje.

Alitaja baadhi ya mambo muhimu ambayo timu hiyo imeshughulikia kuwa ni pamoja na kutoa maagizo katika eneo la mgodi wenye leseni ya uchimbaji mdogo wa madini namba 002211 CWZ, inayomilikiwa na kikundi cha WINIMA, na ambalo ndilo lilihusisha vifo vya watu sita kwa kufukiwa na kifusi, kuwa na mashimo ya uchimbaji 16 tu badala ya 200 yaliyokuwepo awali.

Aidha, alisema kuwa, kwa upande wa eneo la uchimbaji madini linalomilikiwa na kikundi cha Kapumpa, ambalo linahusisha kifo cha mtu mmoja kwa kukosa hewa, kuwa na mashimo ya uchimbaji 15 tu badala ya 177 yaliyokuwepo awali.

“Maelekezo ya kupunguza idadi ya mashimo ya uchimbaji katika migodi husika, yamezingatia usalama wa mashimo hayo kitaalam. Tumeelekeza mashimo yasiyohitajika yafukiwe na kupanda miti eneo husika ili kuruhusu uoto kwa ajili ya kuhifadhi mazingira,” alifafanua Mhandisi Samaje.

Vilevile, alisema kuwa, Timu husika imetoa maelekezo mengine kadhaa kwa wamiliki wa leseni ikiwemo kutoajiri watoto na walevi pamoja na mambo mengine muhimu kama yanavyobainishwa katika Sheria ya Madini.

Mkaguzi Mkuu wa Migodi nchini, Mhandisi Ally Samaje (katikati), akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini wa eneo la Kitunda, lililoko wilayani Sikonge mkoani Tabora, kulikotokea maafa ya watu saba kwa kufukiwa na kifusi, wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa kwanza kulia) hivi karibuni. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri.

Awali, akizungumza wakati wa ziara ya Waziri Muhongo katika eneo hilo la Mgodi, Mhandisi Samaje aliwataka wamiliki wa leseni husika kuzingatia Sheria ya Madini ambayo inawataka kuteua mameneja wa kusimamia shughuli za uchimbaji madini katika migodi yao.

Alifafanua kuwa, mameneja hao wanalazimika kuhakikisha shughuli zote za uchimbaji zinafanyika kwa usalama katika maeneo yao vinginevyo watawajibika kwa mujibu wa sheria.

Shimo la uchimbaji madini katika Mgodi unaomilikiwa na Kikundi cha WINIMA, eneo la Kitunda, lililosababisha maafa ya watu sita baada ya kufukiwa na kifusi hivi karibuni.

Aidha, Mhandisi Samaje aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kuwajibika katika kuhakikisha kwamba wanafanya kazi katika mazingira salama na wanapobaini kuna changamoto katika maeneo yao watoe taarifa kwa viongozi wao na kwa Ofisi za Madini katika eneo lao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, alimhakikishia Waziri Muhongo kuwa atatoa ushirikiano katika kuhakikisha taratibu zote za kiusalama zinafuatwa ili shughuli za uchimbaji madini zifanyike kwa usalama.

Ilielezwa kuwa, ajali katika mgodi husika ilitokea Aprili 20 mwaka huu majira ya saa nane usiku ambapo jumla ya watu sita walifariki kwa kufukiwa na kifusi na mwingine mmoja kufariki kwa kukosa hewa katika mgodi mwingine ulio jirani.

Imeandaliwa na:

Veronica Simba,

Afisa Habari,

Wizara ya Nishati na Madini,

Kikuyu Avenue,

P.O Box 422,

40474 Dodoma,

Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606,

BaruaPepe: info@mem.go.tz,                                             

Tovuti: mem.go.tz